Cover Image
close this bookUtangulizi wa Lugha na Isimu (Tanzania Publishing House Dar Es Salam, 1994, 121 p.)
close this folderSura ya Kwanza: Ujuzi wa Lugha
View the document1.0. Utangulizi
Open this folder and view contents1.1. Kujua Lugha ni nini?
Open this folder and view contents1.2. Isimu ni Nini?
View the documentMazoezi

1.0. Utangulizi

Katika mazungumzo ya kawaida watu husema, kwa mfano, kuwa “Ali na Hadija wanazungumza Kiswahili”, “Esther na James wanazungumza Kiingereza”, au “Mahombwe na Kinyashi wanazungumza Kishambala”, n.k. Bila shaka wakisema hivyo wana maana pia kuwa watu hawa wanajua lugba ya Kiswahili, Kiingereza, Kishambala, n.k. Wakati huo huo, itakubalika kuwa, katika maongezi ya kawaida kama haya, wanaozungumziwa ni wanadamu wa kawaida ambao wamejifunza lugha zao katika mazingira ya kawaida ya kijamii.

Wataalamu wa lugha wanakubaliana, kwa kiasi kikubwa, kuwa mtoto yeyote wa binadamu akifikisha miaka mitano hivi, kama hana dosari zozote katika ubongo wake, na amekulia katika jamii ya watu wanaozungumza lugha fulani, atakuwa amefikia kiwango cha kutosba cha kujua lugha hiyo. Hivyo anaweza kuitumia lugha hiyo katika maisha yake ya kawaida. Wala si lazima lugha hiyo iwe sawa na ile wanayoijua wazazi wake. Ikiwa, kwa mfano, mtoto huyu amezaliwa Uingereza, na hivyo kukulia katika jamii ya wazungumza Kiingereza, basi atajua Kiingereza kama lugha yake ya awali, bata kama lugha ya awali ya wazazi wake ni Kisukuma, Kijerumani, au Kichina. Vivyo hivyo, kama mtoto huyu angezaliwa na kukulia katikati ya jamii* ya wazungumza Kiyao, hiyo ndio ingekuwa lugha yake ya awali. Ni kweli, basi, kusema kuwa kila mwanadamu anao uwezo wa kujua lugha, na matagemeo yetu ni kuwa atajua lugha fulani. Ikitokea kuwa mtoto anafikisha umri wa miaka miwili na hajatamka hata neno moja, tutashuku haraka kuwa mtoto huyo ana matatizo.

Lugha inachukuliwa kama “tabia” ya kawaida kabisa ya mwanadamu, na kwa sababu ya ukawaida huo, si mara nyingi wanadamu watakaa na kujiuliza kitu hiki “lugha” kikoje. Hii ni kwa sababu, kwa desturi, wanadamu hawadadisi sana kuhusu mambo ya kawaida. Kwa mfano, watu wote tunaweza kupumua, lakini ni wangapi kati yetu ambao tunajua lolote kuhusu jinsi mapafu yetu yanavyofanya kazi; tunajua kuwa tunaona kwa kutumia macho, lakini ni wangapi tunayo fununu kuhusu macho yetu “yalivyoundwa”. Hali kadhalika, wote tunajua kuweka chakula mdomoni na kutafuna, lakini wengi wetu hatujui kunatokea nini hasa chakula kinapoingia kinywani mpaka kinapogeuzwa kuwa lishe muhimu ya miili yetu. Lakini pia tunajua kuwa wako watu ambao kazi yao hasa ni kuchunguza maswali haya na kuyatafutia majibu. Hao tunawaita wataalamu. Na utaalamu wao unatuwezesha kuelewa mambo haya, na pia kuongeza maarifa yetu juu ya miili yetu na tabia zetu zinazoonekana za kawaida. Katika sura zinazofuata za kitabu hiki, tutaangalia kwa undani chombo hiki “lugha” ambacho wanadamu wanakitumia katika maisha yao ya kawaida, tukichambue ili tukione kikoje, na kinafanyaje kazi.