Cover Image
close this bookUtenzi wa Nyakiiru Kibi (ECOL Publications, 1997, 109 p.)
View the document(introduction...)
View the documentKutabaruku
View the documentDibaji
View the documentFasilu ya Kwanza
View the documentFasilu ya Pili
View the documentFasilu ya Tatu
View the documentFahirisi
View the documentKinyume

Dibaji

Utenzi wa Nyakiiru Kibi unasimulia historia ya kuanzishwa kwa utawala wa Ukoo wa Babito katika nchi ya Kiziba, wilaya ya Bukoba, katika karne ya 15. Babito walikuwa ni wahamiaji wa Kiluo kutoka Uganda. Walifika Kiziba kutokea Bunyoro nchini Uganda, ambako walikuwa tayari ni watawala. Historia ya Babito katika maeneo haya inaonyesha namna watu wa jamii na lugha mbalimbali hapo kale walivyokuwa na maingiliano na ushirikiano mzuri katika kujenga utaifa na ustawi wao. Siasa za ukabila na ubaguzi hazikuwa na nguvu.

Nyakiiru Kibi alikuwa ni kiongozi wa kundi la Babito lililofika Kiziba, labda kama mwaka 1450. Watu hao waliishi kwa amani na ushirikiano mzuri na wenyeji wao, yaani Waziba. Hatimaye, inasimuliwa kuwa Nyakiiru alishirikiana na Kanyamaishwa, ambaye alikuwa mtoto wa mfalme wa Kiziba aliyeitwa Ntumwa, kumwua mfalme huyo na hivyo kujichukulia madaraka ya utawala. Uzao wa Nyakiiru Kibi umeitawala Kiziba hadi mwaka 1963.

Hadithi ya utenzi huu imetokana na masimulizi ya wazee ambayo yamehifadhiwa katika vichwa vya watu na kupokezwa kwa mdomo tangu karne ya 15. Ni vigumu kwa masimulizi ya aina hiyo kukubaliana kuhusu kila kipengele. Haca hivyo, yapo mambo kadha yamsingi ambayo yanajitokeza karika karibu masimulizi yote. Mambo hayo ndiyo nimeyatumia kama kiini cha utenzi huu. Kazi niliyoifanya ni kuyakusanya masimulizi hayo, kuyachuja, na kuyapanga kisanaa ili kupata hadithi nzuri yenye mshikamano na mtiririko unaofaa, na yenye mafunzo fulani kwa vizazi vya leo. Hivyo utenzi huu hausimulii historia kavu, bali unasimulia hadhithi ya kusisimua inayotokana na historia iliyochanganyika na visakale. Visakale ni masimulizi kuhusu mashujaa wa kale ambayo yamechanganya ubunifu.

Msomaji ataona kuwa katika utenzi huu Ngoma imepewa hadhi kubwa. Hii inatokana na mila ya falme nyingi za eneo la Maziwa Makuu, ambazo hutumia Ngoma kama alama ya utawala. Hivyo kadka tamaduni hizo Ngoma ya utawala ina hadhi sawa na Bendera ya Taifa. Ngoma ya Nyakiiru iliitwa Kachwankizi. Maana yajina hilo ni karibu sawa na “Yenye kukata maini, kubwaga moyo au kumda mtu simanzi kubwa.” Ngoma hiyo inasemekana iliharibiwa vitani katika karne ya 18. Baadaye iliwambwa Ngoma nyingine iliyopewa jina hilohilo na ambayo ipo mpaka leo. Imehifadhiwa katika Ikulu ya mwisho ya Babito iliyoko katika kijiji cha Gera, tarafa ya Kiziba.

Utenzi huu umekusudiwa usomwe na vijana. Hivyo lugha yake imerahisishwa kidogo ili ieleweke vizuri kwa walengwa. Maneno magumu, au matumizi magumu ya maneno ya kawaida, yameelezwa katika fahirisi mwishoni mwa utenzi. Aidha yameonyeshwa kwa chapa ya italiki mahali yalipotokea kwa mara ya kwanza. Maneno ya lugha za asili vilevile yameelezwa katika fahirisi. Kadhalika yameonyeshwa kwa chapa nene yanapotokea kwa mara ya kwanza. Watu wazima na wanafunzi wa madarasa yajuu zaidi vilevile wanaweza kufaidika na utenzi huu. Hao pengine hawatahitaji kurejelea fahirisi.

Namalizia dibaji hii kwa kuwashukuru wazee wote walionisimulia habari hizi kwenye miaka ya 1960 na 1970. Wazee wote hao sasa ni marehemu. Sitawataja hapa kwa majina kwa kuwa ni wengi mno. Nawashukuru pia wataalamu wa historia ya Kiziba ambao vitabu vyao nimevisoma. Baadhi yao ni F.X. Lwamgira aliyeandika Kamalampaka, na Hans Cory aliyeandika Historia ya Wilaya ya Bukoba.

M.M. Mulokozi
Dar es Salaam
10 Februari 1997


Eneo linalozungumziwa katika Utenzi


Ufalme wa Kiziba