Cover Image
close this bookUtenzi wa Nyakiiru Kibi (ECOL Publications, 1997, 109 p.)
View the document(introduction...)
View the documentKutabaruku
View the documentDibaji
View the documentFasilu ya Kwanza
View the documentFasilu ya Pili
View the documentFasilu ya Tatu
View the documentFahirisi
View the documentKinyume

Fasilu ya Kwanza


Taswira

1
Leo nimekusudia
Hadithi kusimulia
Kutoka hisitoria
Ya nchi ya Tanzania.

2
Ni hadithi ya zamani
Ni hadithi ya thamani
Ni mambo yetu ya ndani
Mababu walitwachia.

3
Nimepewa na wahenga
Ndipo nami nikapanga
Halafu nikayatunga
Na nyinyi kuwapada.

4
Ndipo leo nathubutu
Habari za babu zetu
Za kale ya nchi yetu
Vijana kuwaambia.

5
Nianze kuhadithia
Mambo yalivyotukia
Ili mpate sikia
Na pia kuzingatia.

6
Ni simulizi za kale
Za wahenga na wavyele
Waloishi enzi zile
Ambazo zimepotea.

7
Ambazo zimepotea
Pasina na kurejea
Mageni yamefagia
Ya jadi yamefukia.

8
Basi na twende Bukoba
Ufalume wa Kiziba
Nchi ya nyingi rutuba
Na ardhi inayozaa.

9
Zamani yafikirika
Mwaka elufu hakika
Na mia nne kuweka
Ndipo yalipotukia.

10
Enzi hizo za zamani
Kiziba masikanini
Wahenga walisakini
Wakila na kujinywea.

11
Watu hao wa zamani
Walikuwa na imani
Na mila na zao dini
Zikiwaonyesha njia.

12
Wali na Miungu wao
Tofauti na wa leo
Na Mizimu wenye vyeo
Na Mahoka asilia.

13
Walimjua Ruhanga
Muumba nchi na anga
Na kila kinachotanga
Katika hii dunia.

14
Bwana wa tangu na tangu
Asili ya ullmwengu
Mshika tamu na chungu
Mtawala wa dunia.

15
Mungu aliyetukuka
Mungu wa Waafirika
Ambaye hakuumbika
Na hawezi kwangamia.

16
Aishiye Kuzimuni
Na kuona ya nchini
Na kusambaza auni
Kwa wanaohitajia.

17
Hayupo wa kumzidi
Wala wa kumkaidi
Sauti yake ni radi
Na jicho lake ni jua.


Taswira

18
Huona yalofichika
Hushika yasoshikika
Hujua yasojulika
Atoaye na kutwaa.

19
Hako katika majengo
Ya minara na maringo
Na paa zenye migongo
Watu wanayoinua.

20
Hakuhitaji wajumbe
Wa kutuma kwa viumbe
Kwake hapana wapambe
Wote ni sawa sawia.

21
Hakuhitaji mitume
Kwa wake na wanaume
Manabii wenye tume
Pia hakuwatumia.

22
Hakuwa na misahafu
Kwelezawe utukufu
Kurasa vitu dhaifu
Katu hakuvitumia.

23
Misahafuye Umbile
Na vyote vilivyo mle
Milima yenye vilele
Nyota, sayari na jua.

24
Yumo katika miamba
Na maziwa yenye mamba
Na moyoni mwa mgomba
Malikia wa mimea.

25
Vema utamsikia
Katika radi ya mvua
Ngurumo, tufani pia
Vyote alivyoumbia.


Taswira

26
Hana mke hana mwana
Na ndugu wa kuzawana
Yu baba, ndugu na bwana
Kwa watu wote sawia.

27
Ndiye aliumba Kintu
Baba wa wahenga wetu
Ni babu wa kila kitu
Humu katika dunia.

28
Ndiye alimpa mwenzi
Mwandani wake Kikazi
Ili wafanye uzazi
Watu kujaza dunia.

29
Kikazi yu mwanamke
Kintu kawa mume wake
Na dunia ili pweke
Bila mtu kulowea.

30
Ruhanga hakuwa pweke
Ali na Miungu wake
Waume na wanawake
Wakiongoza dunia.

31
Alikuwepo Mugasha
Mungu wa Ziwa Mtisha
Tufani anafurusha
Piaupepo namvua.

32
Na huyu katanda hasa
Kwa Wasukuma ni Ngassa
Kwa Waganda ni Mukasa
Hata Rwanda yuko pia.

33
Naye Muungu mjanja
Ana mguu mmoja
Huishi katika nyanja
Lweru ndo Vikitoria.

34
Mtawala wa ngurumo
Umemena mtetemo
Maziwa na vilivyomo
Bahari, tufani, mvua.

35
Pia bibi Nyakalembe
Wa kilimo na majembe
Mke wa Mugasha kumbe
Mashamba asimamia.

36
Alikuwepo Kasana
Mungu wa wawinda sana
Na aridhi ni dhamana
Yote kaishikilia.

37
Alikuwepo Irungu
Mwenye uta na kirungu
Mapori ya ulimwengu
Yote amejitwalia.

38
Alikuwepo Lyangombe
Bwana wa wachunga ng'ombe
Hutawala kila pembe
Ng'ombe wanapofugiwa.

39
Yupo Kaihura-Nkuba
Mungu-Radi na dhoruba
Mugasha ni wake baba
Nyayo anafuada.

40
Alikuwepo Wamala
Wachwezi awatawala
Yote ndiye huyamala
Watu yakiwazidia.

41
Pia Kagoro mahiri
Naye Muchwezi jasiri
Babaye alomkiri
Ni Wamala nakwambia.

42
Yupo Kilo siyo chuku
Ni Muungu wa usiku
Penye kiza humpiku
Huona bila ya taa.

43
Yupo naye Bibi Kasi
Kilimoni ndiye bosi
Na Bi Rugila ni nesi
Uzazi ndiye hutoa.

44
Nao wengine Mahoka
Wachwezi walotukuka
Japo sikuwaandika
Walihimidiwa pia.

45
Kwisha wataja Wachwezi
Watukufu wenye ezi
Ndipo naianza kazi
Ya wimbo kuwaimbia.

46
Ya utungo kutongoa
Kwa vina kupangilia
Na kunga kufuatia
Kwa mahadhi ya halua.

47
Ni mengi ya kuhadithi
Ya wema na uhabithi
Ya uzazi na urithi
Na ya urafiki pia.

48
Yote kwa ukamilifu
Pia kwa uaminifu
Kwa ufupi na urefu
Nataka kusimulia.

49
Mshike wana wa leo
Nao watoto wajao
Mjue taifa ndio
Hapo lilikoanzia.

50
Mjue zamani hizo
Kulivyokuwa mzozo
Matetano mzomzo
Kwa tumbo kupigania.

51
Mjue pia hakika
Mambo yaliyotukuka
Mazuri ya kupendeka
Mwanzo yaliyotukia.

52
Halafu kale mpishe
Ya leo mlinganishe
Muone kama kasheshe
Zingali zaendelea.

53
Sasa turudi Kiziba
Kwenye nchi ya rufuba
Na waume wa miraba
Na wake wenye kuzaa.

54
Nchi njema ya kuwanda
Ya uzuri wa kutanda
Milima mingi na nyanda
Zenye rutuha murua.

55
Huko zama za zamani
Mwa ziwa ujiranini
Aliishi sulutani
Mkali kupindukia.

56
Jina lake mwenye ezi
Takwambia waziwazi
Ujue na kumaizi
Ni Ntumwa ninakwambia.

57
Na huyu Ntumwa hakika
Uzinzani alitoka
Kiziba alipofika
Nchi akajitwalia.

58
Alimuua maliki
Kwa kumpiga mkuki
Akachukua miliki
Na watu kuwaonea.

59
Alomwua jina lake
Akitwa Mukama Bike
Mukama wadhifa wake
Ni Mfalume sikia

60
Kaingia kwa mabavu
Akatawala kwanguvu
Kwa kazi ali mvivu
Bali siyo kwa kuua!

61
Kunyonga alikujua
Kukata mashingo pia
Kunyonya na kukamua
Pia alipendelea.

62
Alitawala Kiziba
Ndiyo nchi ya Waziba
Wazaao na kubeba
Kwa wingi wa kuzidia.

63
Yali na majimbo mengi
Nchi hii yenye vingi
Kanyigo ndiko msingi
Mukama alikokaa.

64
Mengine Ishozi, Gera
Kayanga, Bwanja na Bwera
Buyango kwa masogora
Na Ruzinga kuishia.

65
Na vijiji vya mpaka
Lukurungo, Bugandika
Katendagulo, Kashaka
Bukoba waelekea.

66
Haya yote ni majimbo
Yenye waume wa tambo
Kanyigo ndicho kiambo
Mukama alipokaa.

67
Kijiji ni Kigarama
Alipoishi Mukama
Kwa ubwana na heshima
Akila na kujinywea.

68
Na kutoka Kigarama
Waona ziwa lahema
Kaskazi kitazama
Buganda waangalia.


Taswira

69
Na mukama kwenye nyumba
Alikula akavimba
Kitambi kikamyumba
Na mashavu kuzidia.

70
Kwa kufuma na kuuma
Kwa husuma na hujuma
Bilahuruma Mukama
Mali akijitwalia.

71
Akiona mwanamke
Mwenye uzuri wa peke
Humuua mume wake
Mke akajitwalia.

72
Watu 'kiwatia ngwamba
Na inazao akisomba
Akinyang'anya mashamba
Ya masikini raia.

73
Na kila anayepinga
Mpumbavu hana kinga
Anakatwa kwa upanga
Hakawizwi nakwambia.


Taswira

74
Basi hata siku moja
Mkewe mzito mja
Alijaliwa faraja
Mtoto kujifungua.

75
Likapigwa la mgambo
Likilia lina jambo
“Ikuluni kuna mambo
Kajifungua malkia.

76
“Malikia mtukufu
Kazaa mwana nadhifu
Mwingine hafui dafu
Kunawiri kazidia.”

77
Ikaenea habari
Kama pepo za bahari
“Malikia wa fahari
Leo amejifungua!

78
“Pigeni nanga nazeze
Pigeni ngoma mcheze
Marimba yakerereze
Mrithi ametokea!


Taswira


Taswira


Taswira

79
“Unajuaje: Huenda
Mwana mema akatenda
Na haki akazilinda
Kiti akikikalia.

80
“Huenda akawa mwamba
Shujaa mwenye kutamba
Kiziba akaipamba
Sifaze zikatangaa!”

81
Kwa hamu na kwa shauku
Wananchi pukupuku
Kutoka huko na huku
Wakaja kushuhudia.


Taswira

82
Wakaja kumsalimu
Maliki aso makamu
Ambaye hajafahamu
Kuwa hii ni dunia.

83
Na magoma yakatika
Na nanga zikanangika
Na watu wakachemka
Kwa furaha kuzidia.

84
Ntumwa akaarifiwa
Mtoto keshazaliwa
Akenda kwa tuwatuwa
Mwanawe kuangalia.

85
Kwa taabu ya uzito
Kenda kwa mjikokoto
Akikita batobato
Nyayo zake kwenye njia

86
Akafika akaona
Mkewe na pia mwana
Kipara akajikuna
Kwa mawazo kumjaa.

87
Akarejea nyumbani
Kufikiri kwa makini
Lipi linayumkini
Mtoto kumtendea.

88
Hapo kaitwa mganga
Ampe mtoto kinga
Asije patwa na janga
Mikasa ya kumuua.

89
Na mganga asisite
Akaleta dawa zote
Ngisha mitishamba yote
Mwana ya kumkingia.

90
“Mwana awe na afia
Asikumbane na waa
Na awe mtu shujaa
Kitu asiyechelea.


Taswira

91
“Akue ahodhi shamba
Akomae awe baba
Ahodhi ng'ombe si haba
Na maziwa kujinywea.

92
“Shambale lirutubike
Ndizi zisilitindike
Mali iwe mwenzi wake
Ashike na kuachia.

93
“Apate wake aoe
Watoto wamzalie
Heshima imfikie
Fahari na nguvu pia.”

94
Baada ya hayo kuwa
Mtoto aliachiwa
Kwa mamaye kulelewa
Maziwa kujinyonyea.

95
Siku zikapanda ngazi
Majuma yakawa myezi
Ikaonekana wazi
Mwana meno yatamea.

96
Tayari meno ya kwanza
Yataka kujitokeza
Katonda twamtukuza
Mizimu, wahenga pia!”

97
Mama akafurahika
“Atukuzwe Mtukuka
Mwana wangu mpendeka
Meno atajiotea.

98
“Mafizi yamekomaa
Sikuze zakaribia
Zakaribianajua
Mwana nilijizalia.”

99
Na yule Ntumwa Mukaina
Hana raha anahema
Mawazoye siyo mema
Kwa mwana aliyezaa.

100
“Huyu mwana anidsha
Anitisha vya kutosha
Bado ninayo maisha
Mrithi sijawania.

101
“Bado kijana kabisa
Tena mtu wa kisasa
Sitaki wanasiasa
Mambo kuyaingilia.

102
“Nani anayeelewa
Labuda akisha kuwa
Atadai kuchukuwa
Kiti nilichokalia?

103
“Afadhali kuzuia
Ugonjwa haujakua
Kuliko kuungojea
Hadi unapozidia.

104
Hadhari kwa mtawala
Ni jambo liso na dhila
Wangapi wafanya hila
Ukama kuunyakua?

105
“Wangapi wanichekea
Sifa wakinipalia
Ambao wangependea
Kiti changu kukalia?

106
“Wangapi wangetamani
Kutwaa usulutani
Mali zangu za thamani
Namashamba kuchukua?

107
“Wangapi rafiki zangu
Watamani kwa uchungu
Kulia chunguni mwangu
Nyama zangu kubugia?

108
“Moyo wa kibinadamu
Nami ninaufahamu
Nimeshashika hatamu
Kamwe sitaiachia!

109
“Ninaelewa hakika
Katu sitadanganyika
Nimekwisha kunyanyuka
Chini sitakurejea.

110
“Mimi bado ni kijana
Bado nitazaa wana
Sasa hivi ni laana
Vifaranga kutotoa!”

111
Na papo hapo Mukama
Kwa amri akatuma
Mganga aitwe hima
Analo la kumwambia.

112
Mganga kupata wito
Akazikoroga kwato
Macho yamuwaka moto
Kwa furaha kuzidia.

113
Kufika akasalimu
Mukama kumheshimu
Kwa adabu na kwa hamu
Kama ilivyo sheria.

114
Na Ntumwa akamwambia
“Mganga nimesikia
U mahiri kuzidia
Kila kitu unajua.

115
“Sasa mimi nina haja
Ambayo nitaitaja
Ndipo hakuita kuja
Mbele zangu kukwambia.

116
Kabula sijaisema
Nataka ahadi hima
Hapa uliposimama
Ya kuwa hutakataa.

117
“Niambie: Uko radhi
Haja yangu kuikidhi
Kwa manufaa na hadhi
Yangu na wote raia?”

118
Na mganga akajibu
“Bwana wajuajawabu
Mimi kwangu ni wajibu
Mukama kutumikia.”

119
Kuisha hayo kusema
Akamwambia Mukama
“Mimi sasa nitasema
Jambo nililokwitia.

120
“Nataka ujitahidi
Kwaakili najuhudi
Kutumia dawa dhidi
Adui yangu sikia.

121
“Adui huyo ni toto
Zao langu la majuto
Nimeota kwenye ndoto
Litaja kunivamia.

122
“Jitoto hilo ni moto
Ni moto wa mtokoto
Kulizaa sina pato
Ila nikuteketea!

123
“Sasa muda umepita
Meno yatanza kuota
Kayazuie kuota
Uachie ya balaa.

124
“Kwa uwezo wako wote
Na kwa dawa zako zote
Hili dmiza upate
Nchi kuniokolea.

125
“Na uende ukijua
Thawabu yakungojea
Mengi nitakupatia
Hiliukinifanyia.”

126
Mganga akaitika
“E walla, E Mtukuka
Yote yatatimilika
Unayoyahitajia.”

127
Kwisha hayo akatoka
Karejea kwa haraka
Na nyumbani akafika
Dawa akajitwalia.

128
Kisha hapo tasihili
Na tunguri zake mbili
Ndani ya kapu la kili
Kaenda kwa Malikia.

129
Kwenye ya mshonge nyumba
Ilozungukwa migomba
Akafika akaomba
Ruhusa akaingia.

130
Kaingia na kuona
Mzazi na wake mwana
Chipukizi nalo shina
Sebuleni wamekaa.

131
Kasabahi kamaliza
Na kisha akaeleza
“Nimetumwa kufanyiza
Dawa zangu za afua.

132
Kanagiza kwa makini
Simba wa humu nchini
Fizi za mwana yakini
Nije kuzinuizia.

133
“Akomae fizi zake
Anawiri kanwa kake
Azungumze acheke
Na matoke kujilia.

134
“Maharage bila wasi
Napia nyama yabisi
Aweze kula upesi
Na ladha kufurahia.”

135
Malkia akaeleza
“Bwanangu namtukuza
Fanyiza unayoweza
Mwanameno kupada.”


Taswira

136
Na muda huo kichanga
Chatabasamu kijinga
Kakitoa kwa mganga
Mganga kakipokea.

137
Kishapo akachukuwa
Aina nyingi za dawa
Sisi tusiozijuwa
Mwenyewe azitambua.

138
Kafunua kanwa kake
Yule mwana wa makeke
Kisha hizo dawa zake
Moja moja kamtia.

139
“Hii dawa ya kukaga
Wachawi wanaologa
Fizi za wana wachanga,”
Kinywani akamda.

140
“Hii dawa ya kunoa
Meno yapate toboa
Mafizi na kutokea,”
Kinywani akamtia.

141
“Hii ya kulainisha
Mafizi kudhalilisha
Meno yapate pitisha,”
Kinywani akamtia


Taswira

142
“Hii ni ya kutobanga
Mipango wanayopanga
Maadui wa kichanga,”
Kinywani akamda.

143
Kamaliza kumtia
Madawa hayo mamia
Maneno kunuizia
Na kisha kumsugua.

144
Kamsugua ugino
Kwa ari iso kifano
Ili ukaote meno
Meno ya kutafunia.

145
Bali kwa siri mganga
Wajuu tu kauganga
Naye mama wa kichanga
Hili hakulitambua.

146
Fizi la juu 'kafanza
Hata akalibonyeza
La chini akalisaza
Hakulishughulikia.

147
“Kua, mwana wangu, kuwa
Kua upate mabawa
Ukaruke kama njiwa
Na mawinguni kupaa.

148
“Kua na uwe shujaa
Adui upate ua
Nchi ipate kujua
Na jinalo kutangaa.

149
“Nakupa yangu baraka
Sudi njema nakuvika
Kua upate lukuka
Katika hii dunia.”

150
Kamganga kamaliza
Mtoto kamuengeza
“Siku kadha utaweza
Nyama kuishambulia.”

151
Kumsifia akisha
Mikono kajipangusha
Tunguri kazifungasha
Kaaga kajiendea.

152
Katoka ajipongeza
“Hakika nimemuweza
Mukama atanitunza
Mengi atanipatia.”

153
Na siku chache kupita
Mambo yakawa matata
Mwana meno amepata
Bali hofu yanada.

154
Meno yanada hofu
Meno yana uhalifu
Meno yanaleta ufu
Kwa Bwana na Malikia!

155
Meno yanaleta dhiki
Meno yatazua chuki
Meno yaleta mikiki
Ya misiba na balaa!

156
“Tazama mkasa huu
Kaota meno yajuu!
Kweli haya ni makuu:
Ni alama ya balaa!

157
“Meno nani kasikia
Ya juu kutangulia
Ya chini hayajangia
Fizini kujitokeza!

158
“Twamhofia Mukama
Ufalumewe mzima
Katu hautasimama
Haya yakiendelea!”

159
Naye yule Malikia
Kuona yalotokea
Akalia, akalia
“Mwanangu wamemuua!

160
“Wameniulia mwana
Kwa kumda laana
Ni heri kuwa kitwana
Kuliko haya kwambua.

161
“Heri kuwa kijakazi
Kuishi kwenye masizi
Kuliko kuwa mzazi
Wa mwana mwenye balaa.

162
“Heri mimi kwangamia
Kuliko kutokomea
Kwa sababu ya balaa
Mwana niliyemzaa!

163
“Na alaumiwe yule
Aliyethubutu vile
kuleta ulozi ule
Mwanangu kumpalia.

164
“E Mugasha mwenye kafi
Mchawi mpige kofi
Aishi maisha ghafi
Afe bado apumua!”

165
Na habari ikatanda
Ikatanda na kuranda
Ikaranda na kuwanda
Nchi yote kuenea.

166
Na magoma yakadunda
Mithili ya debe shinda
Zikapulizwa na panda
Maafa yametokea.

167
Maafa yametokea
Kuichafua dunia
Mtoto wa Malikia
Ndiye mletaji baa!

168
Zikafika sikioni
Mwake Ntumwa kasirini
Akaelewa moyoni
Mganga amepatia.

169
Wakafika vijakazi
Huku walia machozi
Mbele ya kiti cha ezi
Msiba kuutongoa.

170
Mukama akisikia
Ainri akaitoa
Wajakazi kuwaua
Wamemtia fadhaa!

171
Wazana wakauawa
Viungo kukongolewa
Na kuachiwa kengewa
Miambani kujilia.


Taswira

172
Na Ntumwa akasimama
Alia na kulalama
“E Ruhanga! Mungu mwema
Kwa nini kunionea?

173
“Oh! Nisiye na bahati!
Oh! Ningekuwa maiti!
Waseme Ntumwa hayati
Kuliko hiki kuzaa!”

174
Wakasikia raia
Mukama akiugua
Huruma wakamwonea
Kwa yaliyomwangukia.

175
Na wakafika harara
Wazee wenye vipara
Bami walio na ghera
Ya nchi kuiokoa.

176
Wajuao kila mila
Kila ada, kila hila
Wajuzi wenye jamala
Na heshima kwa raia.

177
Kwa majonzi wakafika
Machozi yawadondoka
Miguuni pa malika
Wote wakasujudia.


Taswira

178
Wakasujudu: Hdbuka
Ewe Simba mtukuka
E! Lugaba msikika
Tunakuomba sikia.

179
“Sikiza Mukama wetu
Wasemayo wako watu
Wazee wa nchi yetu
Walezi wa jumuia.

180
“Nchi imeangukiwa
Na balaa bila dawa
Miliki yanajisiwa
Na nafusi yako pia.

181
“Sisi pia tu wazazi
Tuna wana na wakazi
Hivyo twalia machozi
Haya tunapokwambia.

182
“Majonzi yametukaba
Twasakamwa na msiba
Bali mila za mababa
Hatuwezi kwingilia.

183
“Kuingilia ni shari
Mizimu watakasiri
Nchi wataihasiri
Na watu kuangamia.

184
“Hivyo baba tunasihi
Twasihi wako wajihi
Kiri leo asubuhi
Mila yetu kutimia.

185
Akasema mfalume
Pulikeni wanaume
Timizeni hiyo tume
Ya Mizimu wa afua.

186
“Jambo limesha tukia
Baa limetupitia
Pigo limetwangukia
Ni bure kulizuia.

187
Naugulia uzazi
Naugulia ulezi
Vijaluba vya machozi
Vyataka kujifumua!

188
“Hata sasa hali sina
Macho yanisinasina
Ningelia kama mwana
Lakini najizuia.

189
“Ningetamani kulia
Bali ninajizuia
Sulutani akilia
Miliki huangamia!”

190
Wakisikia majaji
Bwana wakamfariji
Kishapo mbele ya taji
Wakajiondokelea.

191
Wakatoka wakaenda
Mioyo inawadunda
Cha malikia kibanda
Wakabisha na kungia.

192
Wakasema: “Leta mwana
Tena kwa haraka sana
Leta mwana wa laana
Tupate kumchukua!”

193
Akabisha Malikia
“Mwana hamtachukua
Kabula ya kuniua
Hapa nilipokalia!”

194
Wakasema: “Hilo mwiko
Sisi tu raia zako
Twataka tunutu lako
Si roho ya Malikia!”

195
Malikia akalia
Machozi kumlowea
“Sikubali nawambia
Mwanangu kunitwalia!

196
“Mnataka kuniziba
Raha tamu ya kubeba
Na kumlea kwa huba
Mwana niliyemzaa.

197
“Furaha ya kuliwaza
Raha ya kubembeleza
Mtoto anapocheza
Mwaja kunizuilia.

198
“Wa heri mama wagumba
Wasiofahamu mimba
Mateso ya myezi saba
Na miwili kwongezea.

199
“Wasiojua ajizi
Na mateso ya ukazi
Na uchungu wa uzazi
Na taabu za kulea.

200
“Heri kutozaa tena
Heri umama kukana
Kuliko kuzaa mwana
Usimwone anakua.

201
“Sikuzaa nimzike
Mwana wangu wa upweke
Bali yeye anizike
Siku itapowadia.

202
“Mzazi kuzika mwana
Ni kipeo cha midhana
Nani tadumisha jina
Lake katika dunia?

203
“Nani takuza ukoo
Kwa kuongeza uzao
Nani tatunza mizio
Na mila za jumuia?

204
Mwanondolea mwangaza
Kwa mwanangu kupoteza
Sasa usoni ni kiza
Maisha yamenishia!”

205
Akalia, akalia
Anga akalipasua
Moyo ukamuugua
Akalia Malikia!


Taswira

206
Wazee wale kwa nguvu
Na kwa mioyo mikavu
Kitoto chenye utuvu
Mama wakamtwalia.

207
Mama kuleta matata
Wakamfunga kakata
Na kumuacha aguta
Alia na kuugua.

208
Nasikuchache kupita
Mauti yakamuita
Roho yake akakata
Kamba akaiachia!

209
Wazee wakasafiri
Nacho kitoto kizuri
Siku moja ya safari
Mpakani wakatua.

210
Wakatua mpakani
Na kwingia mashuani
Kuvuka hadi ng'amboni
Kibumbiro kuingia.

211
Kagera wakauvuka
Na Kitara wakafika
Mila iliyotukuka
Wapate kutimizia.


Taswira

212
Na Kibumbiro wakaja
Nchi ya mti mmoja
Nchi ya vingi vioja
Nchi ya kiu na njaa.

213
Ukingoni mwaKagera
Penye viboko na vyura
Mtoto wakamgura
Kanyigo wakarejea.

214
Wakamuacha mtoto
Alia bila msito
Shingoni hirizi nzito
Ya ukoo kavalia.

215
Na mtoto akabaki
Analia hasikiki
Amezungukwa na dhiki
Navitisho vyadunia.

216
Viboko wananguruma
Vifaru wanakoroma
Mamba wanahemahema
Yeye amejilalia!

217
Hoi kwa njaa na kiu
Kando ya mto mkuu
Macho kayakaza juu
Chali amejilalia.


Taswira

218
Magharibi ikafika
Mtoto amekwajuka
Koo limemkauka
Sauti imepwelea.

219
Gharighari la mauti
Akapita mwana siti
“Yo! Hapakunamaiti!'
Akataka kukimbia.

220
Kuni zikamponyoka
Ambazo amezishika
Yowe likamdondoka
Roho ikamkimbia!


Taswira

221
Bali mtima wa pili
Ukamtia akili
“Kwani kukimbia hili
Nini unachohofia?

222
“Na hata kama ukifa
Huna hasara kwa kufa
Huna tumai la sifa
Wala kuwa Malikia.”

223
Wacha uwoga uende
Udadisi umpande
Akapiga moyo konde
Mtoto akamwendea!

224
Kumfikia kaona
Bado yu mzima mwana
Bado macho yanaona
Na moyo wampapia.

225
Akamwinua kwa wema
Mtoto moto kwa homa
“Mzuri kama Mukama
Huyu mwana angalia!

226
“Atakuwa mwana wangu
Katika uzee wangu
Nitamchukua kwangu
Upweke tanondolea.

227
“Nitamlea vizuri
Nitamfunza ya heri
Atakuwa asikari
Muda atakapokua.

228
“Kichwa kikiwa cheupe
Na maungo chepechepe
Moyo utawa mweupe
Furaha tanipatia.”

229
Kampeleka nyumbani
Kwa shangwe iso kifani
Wakafika majirani
Mwana kumuangalia.

230
Baraza likaitishwa
Azima ikapitishwa
Aitwe Kanyamaishwa
Mwana wa nyika sikia.

231
Yu mtoto wa porini
Kwani kakutwa mwituni
Jina hilo silo duni
Ukweli laelezea.

232
Na mtoto akaishi
Bila mwingi ushawishi
Akawa mtu wa jeshi
Kijana wa ushujaa.

233
Pia akawa muwinda
Msasi katika nyanda
Upinde akaupinda
Podo akajisukia.

234
Na ukipita wakati
Bibi kapatwa mauti
Kama wengine hayati
Waliomtangulia.

235
Kanyamaishwa kalia
Kaburini kamtia
Matanga kamkalia
Kama ilivyo tabia.

236
Kwa upweke akabaki
Mwisho kaona ni dhiki
Katafuta mshiriki
Mke akajiolea.

237
Walakini hakujua
Wapi alikotokea
Nasabaye asilia
Katu hakuitambua.