Cover Image
close this bookMajuto ni Mjukuu (Pheonix Publishers ltd., 1999, 80 p.)
View the document(introduction...)
View the document1. Fahali watatu
View the document2. 'Ole Gatu', kijana wa Kimaasai
View the document3. Kuchakulo wawili
View the document4. Mbwa koko
View the document5. Mbeke, msichcma wa Kikamba
View the document6. Mfalme wa vyura
View the document7. Fisi na mwanang'ombe
View the document8. Kangi na ndugu zake
View the document9. Wambui na chungu cha asali
View the document10. Majuto ni mjukuu
View the documentBack Cover

9. Wambui na chungu cha asali

Karibu na mto wa Mathioya, huko pande za Murang'a, kuna nchi nzuri sana yenye milima na mito ambayo hupita pasipo kukutana. Mito yote huanzia mlima wa Nyandarua na kuungana baada ya maili nyingi na mto mkubwa wa Sagana ulio mto mkubwa kuliko mito yote mingine katika nchi nzima ya Kenya.

Mto Sagana huanzia upande wa magharibi wa Mlima Kenya. Chanzo chake ni vijito vidogo vidogo; hata hakuna mtu awezaye kufikiria kuwa vijito hivyo vinaweza kuwa mto mkubwa kama Sagana. Lakini vikishaungana vyote pamoja, huwa mto mkubwa.

Vijito hivi vidogo kwanza huungana pamoja na kufanya mito midogo, kama Mathioya. Mito hiyo midogo nayo huungana na kufanya mito mikubwa, kama Chania. Mito kama Chania nayo huungana pamoja na kujiunga na Mto Sagana. Wakati unapofika Mto Sagana katika Bahari ya Hindi, huwa umeokota mito mingi. Mto wenyewe huwa na upana wa kama maili moja hivi.

Karibu na mahali pale Mto Mathioya unapoungana na Chania, paliishi mzee mmoja Mkikuyu. Jina lake lilikuwa Kagori. Alipata jina hilo kwa sababu, wakati alipokuwa mdogo, alikuwa akivaa ngozi ya mwanang'ombe. Kazi Kagori aliyoipenda mno ni kutundika mizinga ya nyuki na kukusanya asali, nyuki wakishaitengeza. Nafikiri kila mmoja wenu amepata kusikia kwamba, kabla ya mzee wa Kikikuyu kufunua mdomo wake na kusema lolote juu ya posa ya bintiye, ni lazima kwanza aonje pombe ya asali ya nyuki. Hii pombe hutengenezwa na kijana, au babake kijana anayetaka kuoa.

Desturi hii ya wazee wa Kikikuyu hufanya asali na kazi ya kuikusanya kuwa muhimu sana, na yenye thamani kuu. Kagori, kwa sababu ya kazi hii yake, alikuwa mtu mashuhuri sana. Hata pande za Getwa, wazee wote wenye vijana, walimjua na kumwamini. Kila aliyetaka asali, aliweza kuipata, bila shida yoyote, kutoka kwa Kagori.


Figure

Kagori mwenyewe alikuwa amefanikiwa sana. Alikuwa na wake wawili na wote wakamzalia watoto kumi na wawili. Hata hivyo, hakuna aliyejua ni wangapi, na hakuna aliyejaribu kuwahesabu, kwa sababu si desturi ya Wakikuyu kuhesabu watoto wao. Wao huamini kwamba, kuhesabu watoto ni kama kusema, Mungu amekufanyia vibaya kukupatia watoto wengi, na hii inaweza ikamfanya awachukue.

Kila mwaka baada ya majira ya mavuno, Wakikuyu wote, wake, watoto na waume, huwa na furaha na mashangilio kote nchini. Kila mahali huwaona watu walioshiba, watoto na wanawake wakicheza ngoma zao. Huu ndio wakati kila mmoja anaposikia vile ilivyo vizuri kwa watu wote kumshukuru Mungu (Ngai) kwa kuwapa chakula.

Ni wakati huu hasa ambapo vijana wengi hupenda kuoana. Hili lilimfanya Kagori kuwa na kazi nyingi ya kukusanya asali ili aweze kumpatia kila aliyeitaka, asali ya kutosha. Alitambua kuwa asipofanya hivyo, huenda watu wakasema kwamba amewanyima asali wakati ule wa haja na wakatae kumwamini tena.

Siku moja Kagori alikuwa na chungu kimoja tu cha asali. Mizinga yake yote haikuwa na asali, na ilikuwa ni wakati mbaya sana kwake. Alikichukua hicho chungu na kukiweka juu ya susu aliokuwa ameijenga ndani ya nyumba yake (thingira). Alijua kuwa hakuna yeyote anayeweza kujua mahali alipokiweka.

Wakati wa mchana, wake zake wote huwa wako mashambani, naye Kagori huwa katika baraza la wazee. Wambui, binti wa Kagori na dada zake waliachwa huko nyumbani.

Kama ilivyo desturi ya watoto, Wambui na watoto wengine walianza kucheza mchezo wa kujificha. Wambui, bila kujua, alijificha juu ya susu ya babake. Alipopanda juu yake, alikigusa chungu cha asali. Huko kugusa kukamfanya kuwa na hamu sana ya kujua ni nini kilichokuwemo. Aliinua mkono wake wa kulia na kutumbukiza kidole cha shahada ndani ya mtungi. Alikitoa upesi na kukitia kinywani, huku akisema,

"Hm! kumbe baba ameiweka asali yake hapa?" Mate yalianza kumtoka kinywani kwa utamu mpaka ikamlazimu kutia kidole mara ya pili, ya tatu, na hata ya nne. Alikikunja kidole, ili kipate kukomba asali nyingi zaidi. Kisha akavikunja viwili. Na mwisho akakomba kwa mkono mzima. Hata hivyo, aliona hatosheki na akaanza kula upesi upesi, asije akakutwa na dada zake.

Huko chini, dada zake walikuwa wakimwita kwa sauti kubwa, lakini hakusikia. Fikira zake zote zilikuwa katika chungu cha asali. Kwa bahati, dada walichungulia juu ya susu na hapo wakamwona Wambui amejikunyata.

"Toka, tumekuona," wakasema kwa kicheko na furaha. Wambui hakuwa na haja na mchezo tena. Alichokitaka na alichokifikiria, ni chungu cha asali. Alitoka, huku akificha mikono yake,ili dada zake wasije wakagundua alichokula. Lakini, lo! alisahau kupangusa mdomo wake; na hata kama angeupangusa, harufu nzuri ya asali ilisikika dhahiri puani mwa dada zake.

"Ni kitu gani umekula?" Njoki akauliza.

"Ni asali," Wahu, dadake mdogo, akajibu, hata kabla ya Wambui kusema lolote. Hapo, dada zake wote kwa sauti moja wakaanza kuimba.

"Haiia! Haiia! tutamwambia baba ulikula asali yake. Haia! Haia!" huku wakirukaruka kwa furaha, kama kwamba itakuwa vizuri kuona dada yao akipigwa. Ni desturi ya watoto wote kufurahi, wakiwaona wenzao wamo kwenye matata. Hata ingawa walisema hivyo, huku vinywani mate yaliwatiririka kwa tamaa ya asali. Hakuna hata mmoja asiyetaka kuonja asali kidogo.

"Uliiona wapi asali ya baba?" Wahu akauliza.

"Wataka nikuonyeshe?" Wambui akauliza, huku moyoni akitaka na wao waionje, ili wote wawe wamekosa.

"Ndiyo," dada zake wakaitikia, huku macho yao yakiwa yamekodoka kwa tamaa. Wambui naye akawaeleza pale alipoiona.


Figure

Wote, bila kukawia, wakapanda juu ya susu na wakaanza kuchovya vidole vyao kwenye chungu cha asali. Kila mmoja wao alijaribu kutokula tena, isipokuwa mara hiyo tu, lakini wakashindwa.

Wambui, alipokuwa akitumbukiza kidole kwa mara ya pili, aliligusa tako la chungu.

"Uuui," akalia, "Uuui," akalia tena. "Mumeimaliza asali ya baba," huku akilia kwa hofu. Hapo, wote wakaanza kulia, kila mmoja akisema,

"Si mimi! Ni wewe! Hapana ni wewe," hata mwishowe wakasema kuwa makosa ni ya Wambui, kwani ndiye aliyekula kwanza na akawafanya kusikia tamaa, alipowaonyesha.

Dada zake walianza kuamini kuwa wao hawana hatia. Wambui naye alilia sana kwa hofu na majuto, mpaka macho yake yakawa na rangi ya damu.

Jioni, babake alichelewa sana. Hakufika saa ile ya kawaida. Ingawa Wambui na dada zake walikwenda kulala mapema, yeye hakuweza kufunga macho yake mpaka baada ya muda mrefu. Kila dakika alikuwa akisikiliza kama babake anakuja. Mara kwa mara alisikia kama vile kuna mtu huko nje, na hapo akafikiria ni lazima awe ni babake. Lakini kila wakati ilitokea kuwa si yeye.

Ilipotimu kama saa nne za usiku, babake alifika. "Mbona mmelala mchana?" akaita na sauti ya mtu ameshalewa kwa pombe. Kusikia tu sauti ya babake, moyo wa Wambui ulipiga upesi, pu, pu, pu, pu, kama kuku aliyefungiwa ndani ya tundu. Alitaka kulia, lakini hakuweza. Alinyamaza kimya, huku akijuta sana kwa kula asali ya babake.

Usiku huo babake Wambui hakukitazama chungu chake cha asali. Hata siku ya pili na ya tatu. Lakini siku ya nne, asubuhi na mapema, Ngatia, mzee mashuhuri kutoka pande za Marigi, alifika na kuita, "Kagoori! Kagoori! Mbona mmelala mchana?" Kagori alikuwa anaugua kwa ajili ya ulevi wa kupindukia usiku uliyopita, na aliamka akijisikia amelemewa sana.

"Ni nani?" akauliza, huku akifikicha macho kwa mkono wake wa kushoto.

"Fungua," Ngatia akasema, kabla ya kusema ni nani. Wakikuyu huona haya kujiita majina yao. Ukimwuliza Mkikuyu Ni nani wewe? hukujibu Ni mtu. Hii ndiyo sababu Ngatia hakujibu, alipoulizwa jina lake. Bila kuuliza swali jingine, Kagori aliufungua mlango, na hapo wote wawili wakaamkiana.

"Habari?" Kagori akasema.

"Nzuri," Ngatia alijibu.

"Je, kwenu ni kuzuri?" akauliza Kagori.

"Kuzuri kabisa," akasema Ngatia.

"Kipi kipya huko?" Kagori akaendelea.

"Nipe tumbako kwanza, niamshe pua," Ngatia akasema. Hapo Kagori akatoa kijaluba chake cha tumbako, alichokuwa nacho tangu siku alipotahiriwa; kilikuwa kimegeuka rangi na kuwa chekundu. Alikifunua na kuweka tumbako kidogo kwenye kiganja chdke cha kushoto na kunusa. Baadaye alimtilia Ngatia iliyobaki. Hakuna mzee ambaye anaweza kumpa rafiki yake kitu chochote cha kula, bila yeye kuonja kwanza. Hii ni kama kumwonyesha rafiki yake kuwa hakutia sumu katika chakula, kinywaji au tumbako.

Aliponusa tumbako, Ngatia aliisifu sana kwa vile ilivyokuwa nzuri. Baadaye bila kupoteza wakati, alisema, "Kile kilichonileta saa kama hii, ni taabu zangu. Kijana wangu amefanya uchumba na binti ya Kamau, mzee wa upande wa Gaturi. Pombe ya kupeleka mahari inatakiwa siku ya Ijuma ijayo. Nimekuja kukuomba unipatie asali kidogo ya kuchanganya na maji ya miwa," Ngatia akasema.

"Aaa!" Kagori akasema, huku akijishika kidevu chake. "Mbona ukaja wakati kama huu, na nyuki wameigeukia mizinga yangu? Sijapata kuona wakati mbaya kama huu."

"Tafadhali, usiniambie nirudi mikono mitupu. Nipatie ijapokuwa mkebe mmoja," Ngatia akamsihi. "Sijui nitafanya nini, nikiikosa."

Kagori aliinuka polepole na kutazama juu ya susu lake, ili atoe chungu chake cha asali, huku akisema, "Ninayo asali kidogo tu, ambayo nimemwekea mzee mwingine, ambaye aliniomba nimwekee. Lakini kwa vile najua urefu wa safari uliyoifanya, naona haya kukuacha urudi mikono mitupu."

Kagori alikuwa amekifikia chungu chake na kuanza kukiinua juu. Alishtuka, alipogundua kuwa kilikuwa si kizito kama alivyotarajia.

"Mbona hivi; kuna mtu aliyeingia katika chungu changu?" akauliza huku akikifunua.

"Abaaaaaaba!" Kagori alisema, alipoona kuwa chungu chake kilikuwa kitupu. "Nani aliyekula asali niliyoiweka hapa?" akauliza kwa hasira.

Watoto, ambao sasa walikuwa wameamka na kuketi wakiuzunguka moto, walianza kusema, kila mmoja. "Si mimi. Nami, si mimi," mmoja baada ya mwingine.

"Mnasema si mimi, si mimi, mnafikiri chungu hiki kina kinywa cha kula asali? Tokeni hapa, muniambie ni nani alikula asali yangu!" Kagori akafyatuka.

Bila kujali mgeni aliyekuweko, Kagori alichukua kamba aliyotumia kwa kufungia mbuzi na hapo akawachapa watoto wote sawa sawa. Watoto walipiga mayowe, huku wakisema Si mimi, na wengine wakimshtaki Wambui, lakini baba yao hakusikiliza hayo yote.

Wambui na dada zake walijuta kweli kweli kula asali ya baba yao, bila kupewa. Hawakuthubutu kufanya hivyo tena.