
| Majuto ni Mjukuu (Pheonix Publishers ltd., 1999, 80 p.) |
Hapo zamani palikuwa na mzee, aliyeishi pekee. Nyumba yake ilikuwa mahali pasipokuwa na nyumba nyingine yoyote, na hakuwa akionana na mtu yeyote. Akiishi hivyo alisikia ukiwa sana, hata akataka pawe na mtu, au mnyama, ambaye wangeishi pamoja naye.
Siku moja, alipokuwa amekaa kitako nje ya nyumba yake, kama ilivyokuwa desturi yake kila siku, palipitia karibu mtu mmoja, ambaye naye alifuatwa na mbwa mzuri sana. Alikuwa na madoadoa, na mkia wake ulikuwa umekatwa. Masikio yalikuwa yamesimama wima. Popote mwenyewe alipokwenda, huyo mbwa alimfuata.
Mzee alipomwona mbwa yule, alitamani sana kuwa na wake kama huyo, ili awe akimfuata kila aendapo. Alianza tangu siku hiyo kufikiria vile angepata mbwa wake. Lakini hakupata yeyote kwa muda mrefu.
Siku moja, baada ya kutafuta mbwa kwa siku nyingi, alikuwa amekaa hapo nyumbani kwake, kama kawaida. Alipotazama huko njiani, alimwona mtu mwingine akipita na nyuma yake kulikuwa mbwa wawili, mmoja mweusi na mwingine mwekundu kidogo. Alipoona hivyo, mzee akainuka upesi na kumfuata yule mtu.
"Ewe mpita njia," akasema kwa sauti ya juu.
"Naam," msafiri akaitikia.

Figure
"Tafadhali, nipe au uniuzie mbwa wako mmoja," mzee akamwomba yule msafiri.
"La, siwezi," alijibu msafiri. "Mbwa hawa wangu nawapenda sana, na siwezi kumwachia mtu yeyote. Ukitaka mbwa kwa nini usiende sokoni na kununua?"
"Tafadhali niambie ni wapi sokoni ambako naweza kununua mbwa kama wako," mzee akamwuliza.
"Aa, hio ni rahisi. Ukitaka kununua mbwa, ni lazima utoke hapa asubuhi na mapema, na usafiri kwa mwendo wa maili ishirini, mpaka ulifikie soko la Karatina, na hapo utaona mbwa wengi wanauzwa."
"Vizuri sana, bwana, nitakwenda mpaka huko," mzee akasema.
Mzee alikata shauri, ya kwamba, ni lazima aende mpaka Karatina, akanunue mbwa wake. Kwa vile safari ilikuwa ndefu, ilimbidi kuamka asubuhi na mapema, na kuanza safari yake. Alisafiri kwa mda mrefu, huku akipitia kwenye nchi yenye milima, mito na mabonde. Mfukoni mwake alikuwa amechukua pesa alizofikiria zitatosha kununua mbwa. Alipokuwa amesafiri kwa muda wa karibu masaa saba, akayaona kwa mbali, mabati ya nyumba za Karatina, yaking'aa kwenye jua kali lililokuwa likiwaka.
Alipofika sokoni, alistaajabu sana kuona vile watu walivyokuwa wengi. Kila mahali alipotazama aliona watu wamejaa na akashindwa na kujua vile kila mmoja alijua kule aendako. Alikwenda upesi upesi, ili asionekane kama ni mgeni, asiyejua kule aendako, na kila mara alitazamatazama, kama aweza kuona mahali mbwa wanapouzwa. Alitafuta kwa muda mrefu, bila kuona soko la mbwa, mpaka mwishowe akachoka na ikawa lazima akae chini na kupumzika.
Alipokuwa amekaa chini, alijichukia sana kwa kutolijua vizuri soko la Karatina, kwa maana kama angelijua, labda hangesumbuka hivyo. Ingekuwa vizuri kama angemwona mtu ajuae, amwuulize, lakini watu wote waliopita karibu naye walikuwa wageni kabisa kwake.
Baada ya kukaa chini kwa muda mrefu, aliona ni lazima ajaribu kutafutatafuta tena, na huenda akawa na bahati nzuri na kupaona mahali mbwa wanapouzwa. Kwa kweli, aliona uchungu sana moyoni mwake kufikiria alivyokuwa amesafiri kwa muda mrefu na hata sasa hajawaona mbwa. Alianza kujichukia kwa kutomwuliza msafiri amwelezee vizuri pale mbwa wanapouzwa sokoni. Lakini hakujua ya kwamba soko lenyewe lingekuwa ni kubwa namna alivyoliona alipofika. Alienda huku na huko, bila hata kuuliza mtu yeyote, kwa kuogopa kuwa watajua yeye ni mgeni au ni mjinga. Hali kama angeuliza, hangelichoka namna alivyochoka.
Ilivyokaribia saa kumi hivi, wakati watu wote walipokuwa wakianza kurudi manyumbani kwao, alimwona mtu mmoja, amefuatwa na mbwa watatu, ambao alikuwa amewafunga kwa kamba. Mzee hakuona sababu ya kuwa-funga na hali wote walionekana wakimfuata, bila yeye kuwaburuta.
"Ewe, bwana," mzee akaita.
Mtu mwenye mbwa akaitikia, "Naam."
"Tafadhali niuzie mbwa wako mmoja," mzee akamwambia.
"Nawezaje kukuuzia mbwa wangu na nimewanunua hivi leo? Kwa nini usikimbie sokoni na kununua wako?" mwenye mbwa akamwambia mzee.
"Ni wapi huko wanakouzwa?" mzee akauliza. Mwenye mbwa alistaajabu kuona mtu asiyejua mahali mbwa wanapouzwa, kwa sababu, karibuni kila mtu alipajua mahali hapo. Kwani kila mtu alikuwa na mbwa wake nyumbani. Mbwa aliwekwa ili awe akilinda nyumba wakati wenyewe hawako. "Nenda ile njia ile inayopitia kule, kwenye ule mti mkubwa na ufuate njia iliyo upande wako wa kulia, mpaka utakapoliona duka kubwa lililoandikwa: WATAKA MBWA? NJOO HAPA. Hapo, ukiingia, utaona mbwa wanauzwa," mzee akaambiwa.
"Asante sana, bwana. Nitafanya kama ulivyoniambia," mzee akasema.
Alifuata njia ile aliyoambiwa, lakini, hata hivyo, ilikuwa shida sana kuiona nyumba aliyoambiwa, mpaka baada ya muda mrefu. Alipoiona, aliingia ndani, na mara alipotazama, macho yake hayakuamini alichokiona. Hapo mbele yake walikuwemo mbwa wengi kuliko vile alivyofikiria.
Wengine walikuwa wakubwa, wengine wadogo; wengine weupe, wekundu, weusi, na wenye madoadoa. Mzee alishangaa sana kwa vile alikuwa hajaona mbwa wengi vile.
Alianza kutazamatazama huku na huko kwa muda mrefu, akiona shida sana kujua ni mbwa gani ambaye angemnunua. Na hakutaka kuuliza, ili asicnekane ni mjinga. Baada ya muda mrefu, alimwona mbwa mmoja akimtazama kwa macho ya upendo na hapo akakata shauri ni huyo atakayemnunua. Aliuliza bei yake na mwenyewe akamwambia ni shilingi kumi na tano. Mzee, bila swali lolote, alitoa kijifuko chake cha pesa na kutoa shilingi kumi na tano, akampa mwenye mbwa. Mwenye mbwa alimfunga mbwa na kumpa mzee. Hapo mzee akaanza safari ya kurudi nyumbani. Alifika nyumbani usiku wa manane, lakini hakuona shida yoyote, kwani alikuwa na mbwa wa kumtoa katika hali ya upweke.
Mzee alimpenda mbwa wake kwelikweli. Alimpa kila alichofikiria ni kizuri kwa mbwa. Alimpa nyama na vyakula vingine vizuri kila siku.
Hata hivyo, mbwa hakutosheka. Desturi ya mbwa ya kutaka kutembeatembea, huku akiokota na kunusanusa vitu vichafu, ilikuwa ndani ya moyo wake. Hakuna chakula chochote ambacho kingemfanya akae nyumbani, bila kwenda kutembea.

Figure
Siku moja alipokuwa akitembeatembea huko msituni, aliona paa aliyekufa na mara akaanza kumla. Kumbe, paa yule alikuwa ameuliwa na chui, ambaye alimnyonya damu yake, halafu akaenda kulala kidogo kabla ya kujiburudisha na nyama! Mbwa alipokaa chini kula, hakusikia, huko nyuma yake, chui akimnyemelea polepole. Bila kujua, chui alimrukia mbwa na kumkalia begani. Akamshambulia kwa meno na kucha zake kali, mpaka mbwa akafa. Chui akamchukua na kumpeleka shimoni mwake na kumfanya chakula chake. Nyote mwajua msemo huu, "Chui mzee akila mbwa hurudi kuwa kijana." Kwa kweli chui huyu alirudi kuwa kijana kwa kula mbwa koko.