Cover Image
close this bookMajuto ni Mjukuu (Pheonix Publishers ltd., 1999, 80 p.)
View the document(introduction...)
View the document1. Fahali watatu
View the document2. 'Ole Gatu', kijana wa Kimaasai
View the document3. Kuchakulo wawili
View the document4. Mbwa koko
View the document5. Mbeke, msichcma wa Kikamba
View the document6. Mfalme wa vyura
View the document7. Fisi na mwanang'ombe
View the document8. Kangi na ndugu zake
View the document9. Wambui na chungu cha asali
View the document10. Majuto ni mjukuu
View the documentBack Cover

6. Mfalme wa vyura

Kulikuwako na vyura walioishi katika visima na mifereji ya maji. Waliishi huru kabisa, maana hakuna hata mmoja aliyemtawala mwenzake. Kila mmoja alifanya vile alivyotaka.

Siku moja, walikutana pamoja na kwa sauti moja, wakasema kuwa hawakutaka hali ya kutokuwa na mfalme. Ingelikuwa vizuri kama wangekuwa na mtu ambaye angewaambia la kufanya na kuwakusanya pamoja, wawe taifa kubwa.

Wote pamoja walitazama juu na kwa sauti moja na ya juu wakaomba, "Mungu wetu, twakuomba, kwa hiari yako, utupatie mfalme, atakayetutawala." Mungu alikasirishwa sana na maombi haya, lakini hata hivyo, aliwasikiza na akayakubali yale waliyoyaomba.

Siku moja, baada ya muda si mrefu, walipokuwa wakitafuta na kula chakula chao cha asubuhi, Mungu aliwaangushia kisehemu cha mti mkubwa. Sauti ya mti ulipoanguka majini iliwashtusha sana, na wote wakakimbilia mafichoni. Lakini, muda si mrefu, mmoja mmoja, wakanyemelea mpaka karibu ya mti.

Waliutazamatazama, huku wakiogopa, asije akawa ni adui. Wakagundua kwamba ulikuwa ni mti tu. Wote wakajitokeza na kuukalia juu.

Walitazama juu tena na kumsihi Mungu wao awape mfalme, atakayewatawala na kuadhibu watendao mabaya. Mungu alikasirika sana kwa maombi yao. Hata hivyo, alikubali kuwaletea mfalme.

Baada ya muda kidogo, aliwaletea Korongo kuwa mfalme wao. Korongo alipofika na kuona vyura wengi vile, alifurahi sana. Bila kupoteza wakati wowote, alianza kuwameza vyura, mmoja mmoja. Mfalme Korongo aliwafanya vyura kuogopa sana, walipoona vile alivyowameza wenzao. Wote waliobaki walikimbilia mashimoni, na wote wakalia kwa sauti yenye huzuni, wakaomba, "Mungu Mkuu, twakusihi, kwa neema zako, utuokoe kutoka mikononi na kinywani mwa mfalme huyu gaidi. Mungu, Baba, usipofanya hivyo upesi, bila shaka sisi sote tutaangamia tumboni mwake."

Mungu, kusikia hivyo, akawaita wote pamoja na kuwaambia, "Muliniomba niwaleteeni mfalme wenu. Nilikubali, nikawaletea kijiti cha mti, ambacho hakikua kingeweza kuwafanyia baya lolote. Mlikikataa na kukikalia juu, ili munionyeshe kuwa ni kijiti tu. Mliniomba tena niwape mfalme mwingine. Huyu Korongo ndiye Mfalme wenu. Watu wakipata, hufurahia kile walicho nacho, na kushukuru; lakini nyinyi hamkutosheka na uhuru wenu, wala mfalme asiye na meno. Basi Korongo ndiye mfalme wenu."

Tangu siku hiyo, Korongo hupenda kukaa majini kwenye vyura wengi. Lakini siyo kusema vyura humpenda.