
| Majuto ni Mjukuu (Pheonix Publishers ltd., 1999, 80 p.) |
Zamani za kale Wakikuyu na Wamaasai hawakupendana kama walivyo hivi sasa. Kila mara walikuwa wakipigana. Walioshinda waliteka wake, watoto na mifugo wa washindwa na kwenda nao.
Mara kwa mara vijana wa Wamaasai na Wakikuyu walishikwa mateka vitani. llikuwa kawaida kumkomboa askari aliyetekwa, lakini watoto na wanawake hawakukombolewa. Waliposhikwa na adui, walipelekwa kwa waliowateka na kufanywa mahabusu. Hata hivi leo unaweza kuwaona wanawake wazee wa Kikikuyu katika nchi ya Wamaasai, waliotekwa nyara wakiwa watoto wadogo. Vilevile wako wanaume katika nchi ya Wakikuyu ambao babu zao walikuwa ni Wamaasai.
Husemekana kwamba, kuna wakati mmoja Wakikuyu walijiunga pamoja na kwenda kupigana na Wamaasai. Walisafiri kwa muda mrefu na maili nyingi kabla ya kufika katika makao ya Wamaasai. Walipofika, waliwavamia Wamaasai, bila wao kujua na kuwashambulia vikali. Waliteka nyara ng'ombe na mbuzi, na hata watoto wa kike na wa kiume. Walikwenda nao mpaka nchi ya Wakikuyu na kuwafanya kuwa watoto wao.
Kati ya watoto waliotekwa, palikuweko kijana mmoja, mwenye umri wa miaka kumi na minne. Alikuwa kijana mwenye sura nzuri, nguvu, na akili nyingi. Alipofikishwa katika nchi ya Wakikuyu, alichukuliwa na kiongozi aliyekuwa ameongoza kikosi kilichomteka, naye akamfanya kuwa mwanae, aishi pamoja na watoto wake wengine. Alipewa kila alichotaka; chakula, maziwa yaliyochanganywa na damu, na nyama.

Figure
Kijana huyo, ambaye jina lake lilikuwa ni Ole Gatu, alipewa kazi ya kuchunga ng'ombe wa huyo bwana wake, na ikawa wataifanya kazi hiyo pamoja na wana wa huyo Mkikuyu. Jina la Mkikuyu huyo lilikuwa Kamau na wanawe walikuwa ni Koori na Kamama. Kamama ndiye aliyekuwa wa kwanza, akiwa na umri wa miaka kumi na sita; Koori akiwa na miaka kumi na miwili. Baina yao palikuwako na msichana akiitwa Wangechi. Kama desturi ya Wakikuyu ilivyo, wao huwapa watoto majina ya wazazi wao. Koori ndiye alikuwa mkwewe Kamau. Hivyo ni kusema ndiye baba wa mama yao. Wangechi naye ndiye alikuwa mama wa baba yao, yaani nyanya wa wote: Kamama, Wangechi na Koori. Kamama ndiye alikuwa kama baba wa Kamau.
Hata ingawa Ole Gatu alijulikana kama mwana wa Kamau, yeye alijua kuwa hakuwa baba wala ndugu wala mkwewe Kamau. Kwa hivyo kila siku alijijua kwamba yeye ni Mmaasai halisi kwa damu na hata kwa fikira. Kila siku alifikiria vile angeweza kurudi nchini kwao, kwa wazazi wake. Hata hivyo, ilikuwa ni vigumu kwa kuwa, kila alipokwenda kuchunga ng'ombe, Koori alikwenda pamoja naye.
Alikaa huko akiwa mateka kwa muda wa miaka mingi na kila siku alikumbuka kwamba yeye alikuwa Mmaasai. Kila siku alifikiria njia ya kutorokea na kurudi kwao. Siku moja, alipokuwa akichunga ng'ombe na Koori, alifahamu la kufanya. Alijua ya kwamba, jambo ambalo angelifanya ili aweze kurudi kwao, ni kumwua Koori, wakiwa huko msituni wakichunga ng'ombe. Akishamwua, angeweza kutoroka, bila kujulikana na mtu yeyote, mpaka awe amekwenda kwa mwendo wa maili nyingi. Alifikiria njia bora ya kumwua Koori ni kumzika ndani ya shimo kubwa, ili asionekane tena na wawe wakifikiri labda mnyama mkali ameishawala watoto wote wawili.
Ili amfanye Koori asijue vile alivyonuia kufanya, alimwomba amsaidie kuchimba shimo hilo, wakati wakiwa huko wakichunga ng'ombe. Koori hakushuku chochote na alikubali kumsaidia mwenzake kazi hiyo ya kuchimba shimo. Walipokuwa wakichimba, Ole Gatu alimfundisha Koori wimbo wa Kimaasai, ambao ukitafsiriwa husema hivi:
Chimba chimba chimba,
Wewe mtu mpumbavu,
Shimo lako mwenyewe,
Lako la kukuzika.
Koori hakujua maana yake wimbo huo na bila shaka alipokuwa akichimba alifurahia sana kuimba, kama ilivyo desturi ya Wakikuyu kuimba wanapofanya kazi.
Kila wakichimba futi moja, Ole Gatu alimwambia Koori aingie ili waone ni futi ngapi walikuwa wamechimba. Alilotazamia kufanya ni kwamba shimo litakapokuwa refu kuliko kimo cha Koori, Ole Gatu amchome kwa mkuki, akiwa ndani na akisha kufa, amzike upesi na baadaye atoroke. Koori kila mara alikubali kuingia bila kujua au kuwa na shaka yoyote juu ya lile Ole Gatu alitaka kumfanyia.
Shimo lilichimbwa karibu futi sita na Koori alipoingia, hakuweza kuonekana. Ole Gatu naye akajitayarisha kuuchukua mkuki na kuutupa huko shimoni. Wakati huo, kitu kilitokea ambacho hakuna mmoja wao alikitazamia. Walipokuwa wakichimba bila kutazama upande wowote, ng'ombe mmoja, aliyekuwa na ndama nyumbani, alikwenda mpaka nyumbani, bila wao kujua. Kamau alipomwona, alimwambia mwanae, Kamama, aende akatazame ndugu zake wengine walikuwa wapi. llikuwa makosa makubwa sana kwa mtoto, akichunga ng'ombe, kuachwa na ng'ombe msituni. Kwa hivyo Kamama alitumwa kuchunguza mahali hapo. Aliwasili wakati tu nduguye alipokuwa karibu kuuawa.

Figure
Ole Gatu alipomwona Kamama, alishtuka sana na dhambi yake ikamfanya kufikiri kwamba Kamama alijua lile alilokusudia kulifanya. Hakumngoja. Alipiga mbio akatoroka, asionekane tena.