
| Ham volume 8 - Jarida la mabadiliko na uimarishaji wa sekta ya Afya Tanzania (Wizara ya Afya, 1998, 38 p.) |
Kila Mwaka huwa kunafanyika Mkutano mkuu ambao huitwa mkutano wa Waganga Wakuu wa Mikoa. Licha ya kuitwa hivyo, mkutano huo huhudhuliwa na viongozi toka Wizara ya Afya, Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Manispaa, Waganga Wakuu wa hospitali za Rufaa wa waalikwa wengine kutoka Sekta na Taasisi nyingine. Mwaka huu mkutano huu ulifanyika Mkoani Mtwara kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 2 oktoba 1998.
Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Afya Mh. Aaron Chiduo na kufungwa rasmi na Katibu Tawala wa Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ambaye alikuwa safarini, nje ya mkoa wake. Wageni wengine mashuhuri waliohudhuria mkutano huo, wakikuwapo Naibu Waziri wa Afya, Mh. Tatu Ntimizi, Katibu Mkuu, Mama M. Mwaffisi, ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wake, Mganga Mkuu Dk. G. Upunda na Wakurugenzi wote wa Wizara ya Afya.
Mada kuu ya Mkutano huu ilihusu kuongelea masuala ya utekelezaji wa mabadiliko ya Sekta ya Afya (Health Sector Reform - the way forward). Kama kawaida mkutano huu ulianza kupokea na kujadili ripoti za Mikoa na Taasisi mbalimbali za Wizara ya Afya na baada ya hapo mada mbali mbali zilitolewa kuzumgumzia mabadiliko katika Sekta ya Afya.
Kutokana na taarifa nyingi za mikoa, zilionyesha kwamba vifo vya kina mama na watoto vilikuwa viko bado juu. Pia ugonjwa wa Malaria ulikuwa bado unaongoza katika magonjwa kumi ya mwanzo (top ten diseases) hasa kwa watoto wadogo. Aidha kumekuwepo na mlipuko mkubwa sana wa ugonjwa wa kipindupindu ambao umesababisha vifo vingi. Mkutano ulipendekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na hospitali za Rufaa washirikiane na taasisi mbalimbali ili waandae utarafibu mahsusi wa kina ambao uwe unafanywa ili kupata vyanzo vya matatizo na pia kila mkoa uwe na mpango wa dharura wa kukabiliana na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu.
Nasaha ambazo Mwenyekiti wa Mkutano, ambaye pia ndiye Katibu Mkuu wa Wizara kwa wajumbe zilihusu mambo yafuatayo:
Ili kupambana na rushwa Wajumbe walihimizwa kuweka mabango sehemu za kazi kwa lengo la kuelimisha wananchi kuhusu gharama mbalimbali za uchangiaji, kuvaa vitambulisho, kuwa na vikao na mawasiliano ya mara kwa mara na wafanyakazi na kuweka visanduku vya maoni katika sehemu zao za kazi.
Kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha kwa kuzingatia kanuni na utunzaji wa vitendea kazi
Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe kuwa taarifa za siri za utendaji kazi za watumishi waliochini yao zinawasilishwa haraka Wizara-ni ili zoezi la upandishwaji vyeo liende vizuri.
Hatua za kinidhamu zichukuliwe mara moja dhidi ya nntumishi anapovunja sheria au maadili ya kazi bila woga wala upendeleo.
Mwenyekiti aliahidi kufuatilia upatikanaji wa dawa muhimu kutoka MSD na aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa wawe wanaleta taarifa za dawa wanazopata na wanazokosa.

Baadhi ya Wajumbe Mkutanoni
Mtwara