Cover Image
close this bookUtenzi wa Nyakiiru Kibi (ECOL Publications, 1997, 109 p.)
View the document(introduction...)
View the documentKutabaruku
View the documentDibaji
View the documentFasilu ya Kwanza
View the documentFasilu ya Pili
View the documentFasilu ya Tatu
View the documentFahirisi
View the documentKinyume

Fasilu ya Pili


Taswira

238
Sasa tuvuke mpaka
Tusafiri kwa haraka
Hadi Bunyoro kufika
Buganda kuipitia.

239
Karine zilizopita
Kumi na nne yapata
Bunyoro ilimpata
Mtawalaji shujaa.

240
Shujaa alitukuka
Hadi nje ya mipaka
Shujaa alisifika
Enziye ikaenea.

241
Jina lake ni Igaba
Sulutani mwenye heba
Mtukufu kwa nasaba
Mdshaji wa dunia.

242
Alitawala Bunyoro
Kwa siasa na wororo
Bila kodi, bila mbaro
Bila watu kukomoa.

243
Igaba alimiliki
Na mke wake Njunaki
Mke wa kwanza wa haki
Wana alomzalia.

244
Mwana aliyempenda
Ni Nyakiru mziwanda
Ali fundi wa kuwinda
Na vitani ni shujaa.

245
Nao wana wengineo
Wake Igaba uzao
Wali wengi kwa zidio
Vigumu kukutajia.

246
Wote wazuri kwa sura
Warefu wa umbo bora
Wasoogopa kakara
Nchi yao kutetea.

247
Na Igaba alihozi
Ngoma muhimu za ezi
Yakwanzani Kachwankizi
Baragumu ikilia.

248
Kachwankizi hiyongoma
Yazidi zote heshima
Ni yake yeye Mukama
Igaba ninakwambia.

249
Nyingine ni Kyezailwe
Ndilo jina iitilwe
Kwa ufundi iwambilwe
Kwa kulia yazidia.

250
Ya tatu Ngoma - Tawala
Ni Kalemaitelula
Nzuri isiyo na ila
Ngurumo inapolia.

251
Ya nne ni Nyabatama
Ni goma lenye matama
Hulia na kurindima
Dunia ikasikia.

252
Tabamulibi yatano
Ngoma isiyo mfano
Inapotamka neno
Hatikosi litakuwa.

253
Hizi ngoma zitukufu
Zilikuwa ni wakifu
Hugusi mtu hafifu
Wala kuziangalia.

254
Vema sana zatunzika
Tangu zilipowambika
Daima moto wawaka
Zipate kujiotea.

255
Zina nyumba za pekee
Ambamo zijiketie
Thubutu ukaingie
Kichwa unaziachia!

256
Wapo watu maalumu
Wahusikao kwa zamu
Kukaa nyumbani humu
Ngoma kuzitumikia.

257
Mkuu wao walinzi
Wa Ngoma hizi za enzi
Ni Mutalala mtunzi
Wa siri za jumuia.

258
Sasa tutege sikiyo
Tusikiye mengineyo
Matuko yote ambayo
Bunyoro yalitukia.

259
Nyakiru alipokwenda
Bila kuaga, kuwinda
Sulutani akapenda
Wanawe kuwausia.

260
Hili alipolihisi
Kawaita majilisi
Na watoto wasiasi
Wito wakaitikia.

261
Wakaja wote wanawe
Kila mtu na mjawe
Na sime na mkukiwe
Mihango kuisikia.


Taswira

262
Akawambia “Wanangu
Pulikeni neno langu
Huu ufalume wangu
Ha'wezi kuwatoshea.

263
“Watoto wangu mwajua
Bado wana ninazaa
Uzazi sijaachia
Hata kesho nitaoa.

264
“Kuzaa ndiyo heshima
Ya mume hasa Mukama
Mume siyo mume kama
Hana wana wa kulea.

265
“Hivyo wanangu pulika
Mimi nimeshawishika
Kuwaonya kukumbuka
Nchi inavyosinyaa.

266
“Wakati ninapowaza
Usoni naona kiza
Kwani wana naongeza
Bila nchi kupanua.

267
“Mbele naona matata
Pindipo nikisha pita
Wana mtanza kuteta
Nchi mtaipasua.

268
“Itakuwa kila mtu
Apende awe yeye tu
Mukama wa nchi yetu
Wengine wawe raia.

269
“Basi mimi ninaona
Jambo hili kulikana
Ni vizuri sana wana
Mkaanze kusambaa.

270
“Mkikaa kuzorota
Ukuu hamtapata
Mtatetana kwa vita
Nchi itaangamia.

271
“Basi wanangu haraka
Nendeni nchi kushika
Nje ya hii mipaka
Dola kujikamatia.

272
“Enendeni kwa werevu
Kwa ujanja na utuvu
Ukakasi na mabavu
Hayataweza kufaa.

273
“Mkithubutu kwa nia
Wenyeji kuwavutia
Nchi mtajitwalia
Bila damu kudondoa.

274
“Siri ya kujulikana
Na kupendwa na watwana
Ni kuwapa vya kufana
Matumbo kuwajazia.

275
“Chakula akisha pata
Kabwela hana matata
Kukutii hatasita
Pia kukutumikia.

276
“Kuelewa yawapasa
Serikali ni siasa
Tabasamu la msasa
Laweza kupa dunia.”

277
Kishapo akachukua
Magoma kawapatia
Kila mwana kamusia
Wapi pa kupaendea.

278
Wa kwanza akamwambia
Buganda kupaendea
Kyezaile kaitoa
Kampa kajiendea.

279
Wa pili kamwagizila
Ankole kuitawala
Na Kalemaitelula
Ngoma akampada.

280
Mwingine kamuusia
Ihangiro kuendea
Tabamulibi sikia
Kampa akachukua.

281
Naye wa nne halafu
Kamkabidhi wakifu
Nyabatama takadfu
Karagwe kuelekea.

282
Ikabaki Ngoma moja
Iliyozidi daraja
Ambayo nitaitaja
Ni Kachwankizi sikia.

283
Hii kaing'ang'ania
Kwa huba nyingi na nia
Kwani hakupendelea
Ngoma zote kuachia.

284
Moja alipenda naye
Iweyake atumiye
Iashirie enziye
Aliyoishikilia.

285
Kamkabidhi kijana
Mutalala lake jina
Kasema “Tunza kitwana
Ngoma nakuagizia.”

286
Balangila wakatoka
Ngoma zao wameshika
Na wakaanza haraka
Safari kuziandaa.

287
Wakapata wafuasi
Kufanya jeshi kiasi
Wakaondoka kwa kasi
Enzini kuelekea.

288
Wake zao nao pia
Na wana waliozaa
Wote wakawachukua
Kisha wakajiendea.

289
Ikuluni pakabaki
Yeye Igaba maliki
Na wake zake lukuki
Umati wa malikia.

290
Kabaki na bind zake
Na wana wadogo peke
Na Nyakiiru mpweke
Nyumbani hajarejea.

291
Hata siku zikipita
Nyakiiru kaja kuta
Ngoma wamezikamata
Bila kumbakizia.


Taswira

292
Ghadhabu zikampanda
Akahaha na kuranda
Asiridhi akaenda
Dculu kuulizia.

293
Kamwambia mwenye dola
“Umenifanyia hila
Hunitaki kutawala
Nami nchi kuchukua.”

294
Akasema Sulutani
“Kosa ni lako yakini
Umekawia mwituni
Wenzo nikawausia.

295
“Mwanangu umethamini
Kuzurura maporini
Kama chui na manyani
Kuliko wangu wosia.

296
“Sasa sina Ngoma tena
Ya kukupatia mwana
Kosa ni lako nanena
Wapaswa kulijutia.”

297
Mwana katoka kanuna
Mashavu yamemtuna
Akasema “Budi sina
Ngoma nitajiparia!”

298
Akaenda tasihili
Kwa hasira kweli kweli
Swala hili kujadili
Na Mutalala sikia.

299
Kamwambia, “Ewe mwenzi
Mimi nakwambia wazi
Tuitwae Kachwankizi
Na mengi kujipatia.

300
“Nakwambia Mutalala
Utakuwa mtawala
Maliki mwenye jamala
Na fahari za dunia.

301
“Utawa mtu tajin
Sulutani wa fahari
Na mimi wako waziri
Mwenye kukutumikia.

302
“Niwe Katikiro wako
Naibu wa enzi yako
Mworiaji wa mambo yako
Yawahusuyo raia.

303
“Wote tu vijana kaka
Damu inatuchemka
Kwani hapa kutumika
Na kukaa tunalia?

304
“Fildria Mutalala
We nami tukiamiri
Kikosi cha asikari
Si tutashinda dunia?”

305
Mutalala kusikia
Hayo anayomwambia
Akakubali kwa nia
Wazo akaliridhia.

306
Mipango ikapangika
Yakakusanywa haraka
Masurufu ya nafaka
Wapate kujiendea.

307
Wakatafuta waume
Wenye misuli ya dume
Na wepesi wa umeme
Wataowafuada.

308
Wakapanga siku njema
Nchi yao kuihama
Wakiwa na hisi kama
Nchi hawatarejea.

309
Pia wakawadokeza
Wake zap kuwajuza
Jua litapochomoza
Watakuwa kwenye njia.

310
Hata usiku wa kiza
Bila mwezi kuangaza
Virago wakafungaza
Hao wakajiendea.

311
Wakaondoka wawili
Na wake zao wawili
Na wanaume wakali
Najamaazaopia.

312
Jamaa kama dazani
Za waume wenye kani
Zilikwenda kwa imani
Nyakiru zategemea.

313
Nyakiru ali na mke
Pamwe na mtoto wake
Ishamura jina lake
Mimba aliyefungua.

314
Kikaondoka kikundi
Kiza kiliposhitadi
Muondoko wa kifundi
Kelele hawakutoa.

315
Kwa mwendo wa nyatunyatu
Kamavivuli si watu
Au chui watukutu
Wakenda wananyatia.

316
Mutalala yule baba
Kachwahkizi kaiiba
Kwa milumba kaiziba
Watu wasije ijua.

317
Hata kukipambazuka
Wakawa wameshafika
Karibuni na mpaka
Nchi kuiondokea.

318
Mutalala amechoka
Ngoma ile kuishika
Nzito mno amenyeka
Bali hakuiachia.

319
Nyakiru akimwambia
“Lete takusaidia”
Mutalala hukataa
“Wacha nitajibebea.”

320
Wakaenda, wakaenda
Wakata nguu na nyanda
Wakaenda, wakaenda
Hadi nyayo kuchubua.

321
Wakenda mwendo wa ngisi
Kwa haraka na upesi
Wakata mbuga kwa kasi
Kusini kuelekea.

322
Wakaenda siku nne
Na mnyama wasione
Walau hata senene
Tumboni kujidlia.

323
Pamba imewaishia
Masurufu yote pia
Ya ugali kusongea
Wapate kuubugia.

324
Hawana tena nafaka
Ulezi ulosagika
Wala ndizi kwa hakika
Wapate kujipikia.

325
Vyungu vipo mabegani
Maji yamo vijitoni
Kuni zimo vichakani
Ila chakula udhia.

326
Njaa ikawakeketa
Matumbo kujisokota
Vyungu wakavikung'uta
Bila kitu kwambulia.

327
Wako katika mapori
Nyika wanazivinjari
Bali mnyama wa pori
Haji wakajiulia.

328
Nyoka watupu waona
Na bundi wanaoguna
Bali mnyama hapana
Mwenye nyama ya kufaa.

329
Wapate minofu watu
Japo mibichi si kitu
Wangerarua mitatu
Kuzimia ile njaa.

330
Wakaenda kwa taabu
Kwayo yaliyowasibu
Wakajuta, wakatubu
“Ruhanga tupe afua!”

331
Kawafariji Nyakiru
“Wenzi wangu jikusuru
Giza ni mama wa nuru
Taabu mema huzaa.”

332
Mutalala kabarizi
“Mimi ndiye kiongozi
Nyakiru wacha uchizi
Madaraka kwingilia!”

333
Akapuuza Nyakiru
“Uongozi si udhuru
Udhuru kujinusuru
Siye na zetu jamaa

334
“Damu iliyotukuka
Hadma itajulika
Sasa watu wanataka
Chakula cha kujilia.

335
“Twapaswa kuunganika
Hiinjaa kuizika
Watu wakisha shibika
Swala hilo litangia.”

336
Wakasonga mbele hima
Huku njaa yawauma
Mioyo imewazama
Matumbo yawalegea.

337
Kufika siku ya tano
Wanyonge bila mfano
Kama manyigu viuno
Matumbo yamebonyea.

338
Na walipofikiria
Wataiaga dunia
Usoni kuangalia
Konde wakajionea.

339
Wakona konde azizi
Na masuke ya ulezi
Yapepea waziwazi
Mikono yawapungia.

340
Mutalala akalia
“Suke nenda kujilia!”
Ngoma chini kaitia
Huyo akajiendea.

341
Akenda suke kuvunja
Ili apate kuonja
Akavunja, akavunja
Na kuanza kujilia.

342
Nyuma Nyakiru amri
Katoa kwa asikari
Wote wanaomkiri
Konde kutoingilia.

343
Akaichukua Ngoma
Na kuipakata vema
Tambulisho la Ukama
La hadhi kuijulia.

344
Kasema “Hatutaenda
Kondeni kama makinda
Kuvuna tusichopanda
Kuiba kando ya njia.

345
“Penye mamba pana mto
Penye moshi pana moto
Pana watu penye woto
Na twende kuangalia.

346
“Shamba hili ni la watu
Watatupa kila kitu
Ni unyama siyo utu
Wenyeji kuwaibia.”

347
Mutalala akifika
Tumbo limemuumuka
Kwa Nyakiru katamka
“Ngoma'ngu nirudishia.”

348
Akazidi kudhukuru
“Mwandani wangu Nyakiru
Yapokee mashukuru
Kwa Ngoma kunitunzia.

349
“Sasa nimesha rejea
Tena nimejishibia
Ngoma yangu tarudia
Kama kwanza kuchukua!”

350
Nyakiru kasema “Hasha!
Ngoma umeiangusha
Ukaifanya garasha
Hivyo sitakupatia!

351
“Umeshindwa kujifunza
Ngoma hii kuitunza
Naona utatuponza
Siye na zetu jamaa.

352
“Hakika hutaipata
Hata kama ni kwa vita
Ukitaka panga futa
Ngoma kuipigania!”

353
Akahofu Mutalala
Akaogopa kitala
Karudi kondeni kula
Masuke aloachia.

354
Hakuwakumbuka wana
Mkewe hakumuona
Alichokijua bwana
Ni tumbole kupakia.

355
Na wengine wakashika
Safari hadi kufika
Nyumba zinazokalika
Makazini mwa raia.

356
Akafuatia nyuma
Mutalala anahema
Alia na kulalama
“Nyakiru wanionea!”

357
Wakakuta moja nyumba
Na kukuta mwenye nyumba
Anakomaga milumba
Nyumanju kajikalia.

358
Kawapokea kiutu
Huyu mfadhili watu
Ukarimu wa Kibantu
Wote wakafaidia.

359
Pombe zikaandaliwa
Wakanywa hatakulewa
Na matoke yakaliwa
Matamu kupindukia.

360
Hapo wakapumzika
Hadi keshoye kufika
Kishapo wakaondoka
Safari kuendelea.


Taswira

361
Wakatoka na kijinga
Cha moto kwenye kitanga
Katika mbugu zichanga
Hao wakaendelea.

362
Sasa wamepata nguvu
Matumbo yao mabivu
Pia moto muangavu
Nao wamejitwalia.

363
Wakenda bila kusita
Wasikutane matata
Siku chache zikapita
Kijiji wakafikia.

364
Na nchi hii nanena
Inajulikana sana
Kibumbiro ndilo jina
Wasiojua tambua.

365
Ndiyo imewapa moto
Na chakula motomoto
Kuiua njaa nzito
Iliyowasakamia.

366
Walichofika kijiji
Pia kiliwafariji
Kawapokea mwenyeji
Mama mmoja sikia.

367
Alikuwa ni kijana
Bado ana usichana
Aidha mzuri sana
Suraye inavuda.

368
Alikuwa peke yake
Nyumbani mwamumewake
Mume amekwenda zake
Nyikani kujiwindia.

369
Malaji wakayapewa
Vitu vyema maridhawa
Wakala kukinaiwa
Na matumbo yakajaa.

370
Na pombe-ndizi muruwa
Wageni wakandaliwa
Wakainywa kuinawa
Sana ikawakolea.

371
Wakala matoke mema
Kwa maharage na nyama
Na maziwa ya kukama
Yenye ladha ya pekea.

372
Hata jioni kufika
Mwenye nyumba akafika
Usasini anatoka
Mawindo amechukua.

373
Akawaona wageni
Wameenea nyumbani
Machoye asiamini
Jinsi alivyoshangaa.

374
Alikuwa yu kijana
Wa sura iliyofana
Mwenye mabega mapana
Na saud ya kupoa.

375
Kiunoni lake vazi
Ni ngozi ya mwanambuzi
Mabega yake ya wazi
Shingoni ndumba kavaa.

376
Kichwani ana kofia
Ya ngozi kajivalia
Kanda la mgomba pia
Kiuno kazungushia.

377
Kaja anatabasamu
Wageni kuwasalimu
Kutaka kuwafahamu
Na hali kuwajulia.

378
Wakisha salimiana
Habari kuulizana
Akauliza kijana
Wapi walikozukia.

379
Mkewe akaeleza
Jinsi walivyotokeza
Naye alivyowapoza
Malaji kuwapada.

380
Mumewe kafurahishwa:
“Wageni mwakaribishwa
Naitwa Kanyamaishwa
Hapa ndipo ninakaa.

381
“Huyu ndiye mke wangu
Johari ya moyo wangu
Mwenzi kwenye ulimwengu
Pamwe maisha twatwaa.

382
“Kazi yangu ni kuwinda
Na kulima na kupanda
Ninazivinjari nyanda
Mawindo kufuatia.

383
“Ninalo jicho la nyayu
Na nyayo za mbayuwayu
Hali taka mke huyu
Nyama humtafutia.”

384
Huyu mtu msomaji
Si mwingine muwindaji
Ni yule tu mtupwaji
Kanyamaishwa tambua.

385
Hayo aliposikia
Nyakiiru kamwambia
“Mimi muwindaji pia
Kama wewe nakwambia.

386
“Jina langu Nyakiiru
Amiri wa watu hum
Muepesi wa kudhuru
Mgumu wa kudhuriwa.

387
“Kwa hekima nasikika
Kwa ushujaa nawika
Bunyoro nilikotoka
Wote hunisujudia.

388
“Siogopi binadamu
Sichi wekundu wa damu
Kujeruhi sifahamu
Nikipiga ninaua.

389
“Sitishiki kwa upanga
Au hila za waganga
Janja zao za kijinga
Mimi ninazitambua.

390
“Sichi umeme na radi
Sichi mazimwi kaidi
Sichi majizi ghaidi
Siogopi nakwambia.

391
“Ni mchezo kwangu vita
Kupigana na kukata
Kuteka na kukamata
Kazi hiyo naijua.

392
“Ni mchezo kwangu vita
Sikatwi kamwe, hukata;
Sikamatwi, hukamata;
Siuawi ninaua.

393
“Minri mtoto wa watu
Mpendelea ya utu
Uungwana wa kikwetu
Ukali na ushujaa.

394
“Ajaye kunitiisha
Hujiandaa kmosha
Kuyapoteza maisha
Ama kunisujadia!”

395
Kanyamaishwa kanena
“Nafurahi kukuona
HamH ya kila kijana
Ni kuona mashujaa.

396
“Ni vema kuyasikia
Maneno ya ushujaa
Mimi pia nakwambia
Si mzembe kwa kuua.

397
“Nimevizoea vita
Hupiga bila kusita
Kazi yangu ni kuteta
Mateto ninayajua.

398
“Nafurahi kujuana
Na janadume la mana
Sikuzoea kuona
Wanaume mashujaa.

399
“Karibu usitarehe
Tule tufanye sherehe
Usiku ukibalehe
Tupate kujilaha.

400
“Karibu na watu wako
Tuchanganyishe vicheko
Kufurahi siyo mwiko
Ndiyo raha ya dunia.

401
“Leo na tuchangamke
Kesho mkapumzike
Kesho kutwa tudmke
Mwituni kujiwindia.

402
“Tukashidane wenyewe
Kanyamaishwa na wewe
Mshindi taji apewe
Kama ilivyo sheria.

403
“Tuonenani msasi
Mwenye mikono myepesi
Na miguu yenye kasi
Mwenzie kumzidia.

404
“Nani ajua kulenga
Mshale kuutiringa
Mnyama kumtindanga
Na moyo kumpasua.

405
“Tuone nani asita
Ashindwa kupinda uta
Au ugwe kuuvuta
Ili mshale kutoa.

406
“Nani ashindwa hujuma
Msituni kujitoma
Mnyama kumuandama
Mauti kumrushia.”

407
Neno likakubalika
Ukapitishwa mwafaka
“Naam” wakaitika
Tambo Utajitambua.”

408
Wakala wakafurahi
Wakanywa wakakirihi
Karibu na asubuhi
Chini wakajilalia.

409
Wote wamekwisha lewa
Na hawakujitambuwa
Mutalala kazidiwa
Wengine kuwapitia.

410
Ikafika alasiri
Jua lapungua hari
Giza lanyata kwa siri
Wakanza kujizindua.

411
Wakaamka wakala
Klsha tena wakalala
Ila yule Mutalala
Kabaki anajinywea.

412
Kabaki anajinywea
Mabuyu ayabugia
Tena amefurahia
Ute wamdondokea.


Taswira

413
Hata kukipambazuka
Vitandani wakatoka
Pombe zimeshawatoka
Vinywa wakavifungua.

414
Wengine wakenda nje
Hewa njema wakaonje
Na vikuni wakachanje
Na watu kusalimia.

415
Wengine wakabakia
Palepale waongea
Porojo waporojoa
Furaha imewajaa.

416
Na Mutalala kabaki
Akijipiga mswaki
Kwa nyama iliyobaki
Usiku walipojia.

417
Ila wawinda mahiri
Kanyamaishwa hodari
Na Nyakiiru jasiri
Silaha wakachukua.

418
Wakachukua silaha
Wamejawa na furaha
Wakaenda kwa madaha
Nyikani kujisasia.

419
Wakenda na mbwa zao
Wawindaji wenzi wao
Mabingwa sana kwa mbio
Amini ninakwambia.

420
Nayo ngoma Kachwankizi
Nyakiru kamkabizi
Mke wake huyu mwenzi
Vema kuiangalia.

421
Asimruhusu mtu
Kuigusa katukatu
Haigusiki na watu
Ila yeye kamwambia.

422
Wakaingia porini
Kwenye nyama kila fani
Wakapanga miadini
Kisha wakatokomea.

423
Kila mtu njia yake
Akashika kwa upweke
Wawinde kisha wafike
Mahali pa miadia.

424
Warejee miadini
Muda ng'ombe malishoni
Warudipo kijijini
Mazizini kurejea.

425
Mwenye mizoga zaidi
Yu mshindi hana budi
Ndiye mwindaji wahedi
Mwenzie kumzidia.

426
Wakashika zao njia
Mwitu kuuingilia
Wanyama kujiwindia
Na sifa kujiletea.

427
Hata ukifika muda
Wakarejea wawinda
Wajifcokota kwa shida
Kwa mawindo kuchukua.

428
Walipoahidiana
Muda waliopatana
Wakafika kukutana
Mshindi kumtambua.

429
Mizigo wakaitua
Wahema na kupumua
Wasiweze kuamua
Mshindi kumtambua.

430
Kila mtu ameua
Wanyama kupindukia
Mizoga imebakia
Huko walikowindia.

431
Wakarudi huko wima
Kuwahesabu wanyama
Wasimalize tazama
Usiku ukaingia.

432
Wakashikana mikono
Wakasifiana mno
Wakafika mapatano
Kuwa wote mashujaa.

433
Kuwa wote walingana
Kwa ufundi wapatana
Wa kuzidia hapana
Hoja wakairidhia.

434
Kisha wakamba kwa nini
Wasifanyane wandani
Urafiki wa chaleni
Wa vitovu kuchanjia.

435
Wakakubali kwa hamu
Kuwa rafiki wa damu
Kila palipo ugumu
Wapate kuuondoa.

436
Buni kavu wakapata
Na kisu wakakamata
Vitovu vyao kukata
Udugu kuuingia.

437
Pekee bila shahidi
Usiku umeshitadi
Watoleana ahadi
Wasizoweza tangua.

438
Mwanga wao mbalamwezi
Shahidi wao ni mwezi
Kiungb ni damu hizi
Watakazozichangia.

439
Sala wakazitongoa
Tambiko wakazitoa
Zipate kuwafikia
Miungu wenye afua.

440
Kisha wakajizatiti
Kwa hamu pia kwadhati
Kiungo cha damu kati
Yao wote kuundia.

441
Wakachanjana vitovu
Wasijalimaumivu
Kadka yale makovu
Buni kavu wakada.

442
Nyakiiru kala buni
Yenye damu ya mwandani
Kanyamaishwa mtani
Udugu kuuingia.

443
Na mwenziwe vilevile
Akaila buni ile
Iliyo na damu tele
Ya Nyakiru suhubia.

444
Buni zilipobugiwa
Kitu kimoja wakawa
Wao na wao wazawa
Vizazi vyote sikia.

445
Wakaahidi kwa dhati
Kushirikisha bahati
Hadi wakati mauti
Mmoja yakimwondoa.

446
Kishapo wakarejea
Furaha imewajaa
Na siri hawakutoa
Nyoyoni walitunzia.

447
Toka hapo kila siku
Huenda huko na huku
Kwa shirika na shauku
Nyama wakijiwindia.

448
Mmoja akiumia
Mwenziwe anaugua
Wote wanadidimia
Kwa maradhi kuingia

449
Na ikawa siku moja
Wakiwinda kwa pamoja
Waliona chaka moja
Mnyama ameingia.

450
Kwa nadhari ya usasi
Walifarakana kasi
Pande mbili kuzisasi
Kichaka kuzungukia.

451
Walikwenda kwa haraka
Mbwa wao wanabweka
Majasho yanawafuka
Ndimi zimeninginia!

452
Walikwenda kwa hadhari
Silaha zao tayari
Tamthili asikari
Majanga kukabilia.

453
Kwa mwendo wa nyatunyatu
Kwa macho ya matumatu
Chaka lote kama chatu
Wawinda walizingia.

454
Kwa hadhari ya kutosha
Bila hofu ya maisha
Silaha wamezinyosha
Hao walijisasia.

455
Hawakuhofu chochote
Kwa sababuwako wote
Na kama chanda na pete
Pendo limewafungia.

456
Muda si muda kupita
Mbwa wakanza kirteta
Nyakiru mara kasita
Macho akayakodoa.

457
Tahamaki akahisi
Nywele zanimka kasi
Pana hatari halisi
Kijana akatambua.

458
Pana hatari thabid
Lazima ajizatid
Woga nyumba ya maud
Kila mwinda anajua.

459
Hajajizadd veroa
Mbeleye akajitoma
Chui anayenguruma
Kwa hamu ya kumuua!

460
Akawachia mshale
Ukenda bila kelele
Shingoni mwa chui yule
Ukabisha na kungia.

461
Chui kapandwa ghadhabu
Kuona yamemsibu
Huyu mtu kuadhibu
Moyoni akaamua.

462
Kajiamulia nduli
Kumuadhibu vikali
Huyu kibahaululi
Aliyemuingilia.

463
Akaruka akapaa
Mataya kayatanua
Kufumba na kufumbua
Mwinda amemwangukia!

464
Mwinda amekuwa mwindwa
Akaribia kupdndwa
Nani atakayeshindwa
Sikia nitakwambia.

465
Mtu anapofungua
Usimwambie toboa
Ya ndani utayajua
Wajibu ni kungojea.

466
Yule chui alituwa
Begani pa mwinda juwa!
Papo akamraruwa
Minofu kumuopoa!

467
Nyakiru akaanguka
Mkuki alioshika
Vizuri kampachika
Adui penye kifua.

468
Na mbwa wakakupuka
Bwabwa bwabwa wakabweka
Chui akababaika
Alia na kuugua!

469
Kanyamaishwa sikia
Huko alikosalia
Rabusha ikamjia
Kuna mambo akajua.

470
Kakimbia kwa haraka
Ananyapa kama paka
Akimwita mpendeka
“Nyakiru naja tulia!”

471
Nyakiru akasikia
Kasema akiugua
“Dude limenidandia
Rafiki ninakwambia!”

472
Kanyamaishwa kuona
Chui, kasema “Hapana
Mzee nitakuchuna
Leo utanitambua!

473
“Leo nitakucharaza
Kwa rafiki kuumiza
Yahe nitakwangamiza
Usipembeze mkia!”

474
Papo huyo! Akaruka
Chui naye akaruka
Wakakutana shirika
Hewani walikopaa!

475
Wakapigana kikumbo
Hawa viumbe wa tambo
Na kukunana matumbo
Ghadhabu zimewajaa.

476
Halafu wakabwagika
Wote wamekasirika
Chui mara akaruka
Makucha akamtia!


Taswira

477
Makucha akamda
Kanyamaishwa sikia
Mguuni yakangia
Kijana akaugua.

478
Kwa hamaki na fadhaa
Nyakiru akajizoa
Mkuki akainua
Adui akamtia!

479
Ukamuingia chui
Akajiona yu hoi
Unamutoka uhai
Maud yanamjia.

480
Akaanguka mwereka
Aridhini kabwagika
Lege mtoto wa nyika
Nguvu zimemuishia.

481
Mbwa wakamrukia
Kwa kiu ya kurarua
Macho wakayaopoa
Na kumtafuna pua.

482
Na wawinda wanadamu
Hali wanatokwa damu
Wakanza kujifahamu
Hali zao kuzijua.

483
Wakaanza kugangana
Madonda kufungiana
Na mikono kupeana
Ya pongezi na heria.

484
Nyakiiru katamka
“Umeniokoa kaka
Sana nitakukumbuka
Hadi mwisho wa dunia.”

485
Kanyamaishwa kakana
“Haki kusifiwa sina
Kwani nisingalipona
Kama si yako afua.”

486
Wakashikana vijana
Na wakakumbatiana
Huku wanasifiana
Na kupongezana pia.

487
Kwa furaha na uchovu
Kwa nderemo na utuvu
Bila kujali makovu
Nyumbani wakarejea.

488
Waganga wakatafutwa
Na madawa yakaletwa
Mahali walipokatwa
Tiba wakawatilia.

489
Siku chache zikapita
Ahueni wakapata
Madonda yakajifuta
Hali zikawarudia.

490
Wasisite wakataka
Silaha tena kushika
Kurudi kwenye machaka
Wanyama kufuatia.

491
Furaha ya muwindaji
Si kukaa kwenye mji
Bali mwituni kuhiji
Hatari kukabilia.

492
Furaha yake msasi
Ni kupigana na fisi
Na kukimbizana kasi
Na ng'ombe-mwitu na paa.

493
Kukabili vya kutisha
Kuua au kufisha
Ndiyo ya mwinda maisha
Naye ayafurahia.

494
Kuzama kwenye mabwawa
Misitu kuitatuwa
Hayo mambo ndiyo sawa
Kwa msasi asilia.

495
Basi wakarudi tena
Kwenye nyika kutetana
Kusaka na kushindana
Na yitu yyenye mikia.

496
Na wakati wote huu
Mutalala yuko tuu
Kila saa ana kiu
Kila saa ajinywea.

497
Hatoki nje ya nyumba
Kazi kula na kuvimba
Tumbo limesha myumba
Kitambi chaning'inia.

498
Haamki akilala
Hadi saa za chakula
Na kishapo halahala
Mapombe hujipakia.

499
Na Banyoro wengineo
Walioacha makwao
Wameshapata makao
Mashamba wajilimia.

500
Nchi hii Kibumbiro
Imeshakuwa Bunyoro
Wamesahau utoro
Kwa furaha walowea.

501
Waishi na hawa watu
Na kuazimana vitu
Hawabaguani katu
Wote wa sawa sawia.

502
Na vivyo hivyo miaka
Ikaja na kuondoka
Kwisha matano masika
Bado hapo walowea.

503
Walakini Nyakiiru
Moyoni hayuko huru
Bado tu anadhukuru
Madhumuniye na nia.

504
Siku moja wakiwinda
Mbali sana waliranda
Wakavuka zote nyanda
Hadi mto kufikia.

505
Mto ule wa Kagera
Mrefu kutia fora
Wenye samaki na vyura
Ndio waliofikia.

506
Watambaa kama nyoka
Toka wa Rwanda mpaka
Na kuenda kumwagika
Ziwani Vikitoria.

507
Ziwani wajichomeka
Na kupita na kuvuka
Na kwenda kuporomoka
Huko Jinja kupitia.

508
Sasa ndo Nili dhahiri
Uhai wa Wamisiri
Wapeleka furifuri
Rutuba kuwaokoa.

509
Waliufika vijana
Mto unaogawana
Nchi zisizofanana
Kiziba na Missenyia.

510
Kiziba ina milima
Na mabonde ya kuzama
Udongo mweusi mwema
Migomba unailea.

511
Ina misitu mipana
Wanyama waonekana
Na vijito vingi sana
Nchini vimeenea.

512
Bali Missenyi hapana
Iko tambarare sana
Udongo wanatiana
Wafaa kufinyangia.

513
Mashamba mengi haina
Bali nyika za kufana
Wanyama kila aina
Kotekote watembea.

514
Ni kame imekauka
Maji yanaadimika
Ila siku za masika
Maji yanaifukia.

515
Basi hawa walikwenda
Kanyamaishwa muwinda
Na Nyakiru mziwanda
Kagera wakafikia.

516
Vijana walisimama
Ukingoni kutazama
Nchi yenye kilajema
Kiziba wakangalia.

517
Akaiona Nyakiru
Macho yakang'aa nuru
“Nchi hii iko huru
Lazima taiendea.


Taswira

518
“Kutawala nimekuja
Styo maisha kufuja
Nchi hii yaningoja
Kipi nakisubiria?”

519
Akaona nchi nzuri
Yenye miti furifuri
Na nyasi kama hariri
Kwa madaha zapepea.

520
Akaona na mashamba
Maridhawa ya migomba
Mikungu yayumbayumba
Ndizi zinajipogoa.

521
Akaona mito bora
Sehemu zote za dira
Chemchemi za kufura
Kwa maji yenye ladhia.

522
Hadi wa macho upeo
Kulienea mazao
Migomba bila kituo
Kaona imezagaa.


Taswira

523
Naye alipotazama
Moyonimwe akasema
“Lazima niwe Mukama
Kiziba kujitwalia.

524
“Lazima nikakamke
Mkuki wangu nishike
Nidhuru na nidhurike
Nchi kujinyakulia.

525
“Kabula sijajifia
Kachwankizi ninajua
Kizibani italia
Bunyoro ilivyolia.

526
“Italia kutangaza
Kwenye vijiji na saza
Ya kwamba limechomoza
Lake Nyakiiru jua.

527
“Italia kujulisha
Enzi mpya za maisha
Italia kutingisha
Misingi ya asilia.

528
“Italia na kunena
Ametawala kijana
Nyakiru Mukama sana
Sikilizeni raia!

529
“Italia kwa mpwito
Ametawala Mbito
Ndiye atawasha moto
Enzi mpya kuzindua!”

530
Nyakiiru kaeleza
“Rafiki yangu nawaza
Kuenda kujitangaza
Mukama huko sikia.

531
“Wajua nilikwambia
Kwako nilipoingia
Kuwa ninadhamiria
Jambo kuu kufanyia.

532
“Kuwa ninaleta vita
Hekaheka na matata
Ngoma yangu kuikita
Mahali panapofaa.

533
“Kuwa ninaleta moto
Kuteketeza maoto
Kutimiza yangu ndoto
Naja mambo kupindua.

534
“Kuwa naja na upanga
Siyo zeze wala nanga
Naja wengine kufunga
Na wengine kufungua.

535
“Hiyo ndo yangu radba
Ewe rafiki sahiba
Tuambatane Kiziba
Kutimiza hii nia.

536
“Panga zetu tuzishike
Na mpaka tukavuke
Tuwazulie makeke
Makabaila sikia.

537
“Twende tukinyatanyata
Kaumu tukiivuta
Kisha tuanze kukata
Wanaotuingilia.”

538
Akakataa mwenzie
“Jama usinitanie
Vipi nikaiwachie
Aridhi ilonilea?

539
“Hapa nimepakulia
Hapa hapa nitafia
Japo walionizaa
Sijui walikofia.

540
“Niombe niue simba
Kukuridhisha mjomba
Niombe kuvua mamba
Yote nitakufanyia.

541
“Niombe kukatakata
Mwili wangu sitasita
Bali unayoyaota
Vipi nitayaridhia?

542
“Kaka mpenzi sahiba
Usinitie msiba
Kutaka nende Kiziba
Nchi yangu kuachia.

543
“Hapa kuna nyanda tele
Na nyika za mtelele
Wanyama nyumanambele
Lipi tena wawania?

544
“Tembo na ngiri na nyati
Wazonga chini ya miri
Samaki wenye madd
Mtoni wamezagaa.

545
“Chakula ki maridhawa
Ulezi tunapakuwa
Twanywa mapombe twalewa
Na matoke twabugia.”

546
Na Nyakiru kwa uchungu
Kasema “Ewe mwenzangu
Ni radhi kula ukungu
Kid nimekikalia.

547
“Nia yangu si chakula
Mimi siyo Mutalala
Sikiliza yangu sala
Ninakuomba sikia.

548
“Sitaki kwenda pekee
Siwezi kwenda pekee
Wawili, wamba wazee
Hawapotewi na njia.

549
“Nakusihi sana kaka
Kwa nadhiri tuzoweka
Na damu zizomwagika
Wawili kutuungia.

550
“Kumbuka mapenzi yetu
Kumbuka ahadi zetu
Vitovu na damu zetu
Jaribu kukumbukia.

551
“Ukikataa rafiki
Kiziba siendi haki
Hapa hapa nitabaki
Kwa huzuni kujifia.”

552
Hayo alipomwambia
Kanyamaishwa sikia
Moyoni yakamwingia
Na jibu akalitoa.

553
“Niwie radhi mwenzangu
Wacha kuwa na uchungu
Uhai huu si wangu
Hili unalitambua.

554
“Maisha yangu ni yako
Yako ni yangu si yako
Kufarakana ni mwiko
Heri kuacha dunia.

555
“Ukifa sitabakia
Namimi nitajifia
Tutaiacha dunia
Pamoja ninakwambia.

556
“Kama una kubwa hamu
Ya Kiziba kufahamu
Enzini kusitakimu
Siwezi kukuzuia.

557
“Ni radhi bila madai
Kuiacha nchi hii
Ni radhi kwacha uhai
Hajayo kuiridhia.

558
“Ni radhi kuacha nyanda
Na wanyama wa kuwinda
Nchi ninayoipenda
Ili wewe kwandamia.

559
“Ili wewe kwandamia
Ukapate kutulia
Upate kujipatia
Lile unalowania.

560
“Upingacho nitapinga
Utengacho nitatenga
Ufungacho nitafunga
Twishi na kuangamia.”

561
Hayo akiyasikia
Nyakiru yakamwingia
Machozi akayatoa
Na Kanyamaishwa pia.

562
Wakalia kama wana
Huku wakumbatiana
Wakalia tena sana
Mwishowe wakatulia.

563
Nyaldru kwa moyo wazi
Akamshukuru mwenzi
Akasema, “Sasa kazi
Ndiyo iliyobakia!”

564
Wakarejea nyumbani
Mali zao za thamani
Wakafungafungasheni
Tayari kujiendea.

565
Mutalala haridhiki
Kwondoka pale hataki
Na pale peke kubaki
Hawezi kuvumilia.

566
Kakubali kidhaifu
Kwa mengi majikalifu
Kuenda safari ndefu
Asiyoipendelea.

567
Wengine hawakusita
Habari walipopata
Wakafunga marobota
Tayari nanga kung'oa.

568
Nawake zao sikia
Na watoto wao pia
Na mali waliyotwaa
Kwao walipotokea.

569
Na silaha zao zote
Nyuta na mikuki yote
Na mitemba yao yote
Ugoro, tumbaku pia.

570
Podo zao mabegani
Sime zao makwapani
Na mikuki mikononi
Nyakiru wakamjia.

571
Wakamba “Tupo tayari
Sisi wako asikari
Ugenini kusafiri
Pia kukuhudumia.”

572
Nyakiru akipulika
Moyo ukaburudika
Kamba “Vema kina kaka
Kesho nanga tunang'oa.”

573
Mitumbwi wakanunua
Kumi haikupungua
Masurufu wakatia
Watayoyahitajia.

574
Wakakusanya mikunga
Ya ndizi kwenye matenga
Na ulezi wakatwanga
Na nyama wakachukua.

575
Wakavifungasha vyungu
Vibuyu mafungufungu
Na miba ya nungunungu
Dawa ya kujikingia.

576
Haya wakisha chukua
Alifajiri sikia
Na Ngoma wakaida
Katika mtumbwi pia.


Taswira

577
Na humo wakaingia
Kanyamaishwa sawia
Na Nyaldru na jamaa
Wake na watoto pia.

578
De mitumbwi mingine
Wale waume wengine
Wambiwa wajigawane
Mtumbwi watu kadhaa.

579
Wakajipakia wote
Pia vitu vyao vyote
Na jamaa zao zote
Vyombo vyote vikajaa.

580
Mutalala amekaa
Mtumbwini kwa fadhaa
Chombo kikiinamia
Hulia: “Twaangamia!”

581
Na safari ikauma
Vyombo vikaenda hima
Vyaibuka na kuzama
Mkondo kufuatia.

582
Ni mkondo wa Kagera
Uendao kwa hasira
Kingo ukiteka nyara
Ziwani ukifukia.


Taswira

583
Magharibi ikifika
Walikuwa wamefika
Mto unapojizika
Ziwani Vikitoria.

584
Wakauacha mkondo
Mitumbwi yao ya mwendo
Wakaiegeza kando
Ufukweni wakatua.

585
Wakapiga kambi yao
Na kukoka myoto yao
Wapike chakula chao
Wale na kujilalia.

586
Wakaziratibu zamu
Adui 'siwahujumu
Bali Mutalala zamu
Hawakuimpangia.

587
Wakisha jia kijio
Wakapewa malalio
Jamaa sehemu yao
Wote wakajilalia.

588
Kanyamaishwa mpole
Na Nyakiru mteule
Waliamua walale
Pahali pamwe sikia.

589
Ja wana wa tumbo moja
Walilala ngozi moja
Ngoma wameipambaja
Hifadhi kuipada.

590
Walilala ngozi moja
Na wake zao pamoja
Na mwana wao mmoja
Ishamura nakwambia.

591
Hivyo walipumzika
Hadi kukapambazuka
Halafu wakaamka
Safari wakaandaa.

592
Mitumbwi wakaishua
Mali wakazipakia
Na wao wakaingia
Safari kuendelea.

593
Na papo wakajiona
Kwenye lile ziwa pana
Limekaa kiungwana
Majiye yametulia.

594
Humu huishi Mugasha
Radi anayeangusha
Na tufani kuzirusha
Kwa waletao udhia.

595
Wakaitoa kafara
Buni kavu kwa ishara
Kwamba hawaji kukera
Bali tu wajipitia.

596
Wakaitoa kafara
Wasipatwe na madhara
Na wakashika majira
Kusi wakageukia.

597
Kwenye majira ya kusi
Wakenda mwendo kiasi
Wakiiandama nsi
Ufuko wafuatia.

598
Wakawasili Kiziba
Jua halijajiziba
Na papo likajiiba
Upeoni kupotea.

599
Mitumbwi wakaegeza
Ufukweni kwa mwangaza
Wa mwezi uliokoza
Kambi wakajipigia.

600
Asubuhi na mapema
Wenyeji wakaja hima
Roho zimewasimama
Wageni kuwangalia.

601
Na wakasema wageni
“Sisi wasafiri duni
Twambieni majirani
Wapi tumepafikia?”

602
Wambiwa, “Wanyamahanga
Hapa paitwa Mitaga
Wakazi wake hutega
Samaki katika ziwa.

603
“Mwote humu ni Kanyigo
Ni nchi kubwa si ndogo
Ina mali na mifugo
Na wakazi kwa mamia.

604
“Ufalume ni Kiziba
Nchi ya walioshiba
Mtawala wetu baba
Kigarama katulia.”

605
Wakauliza wageni
“Rafiki twelekezeni
Njia ya kwenda mjini
Kigarama kuingia.”

606
Na papo wakaambiwa
Kulifuatia ziwa
Waende bila kutuwa
Kijiji watafikia.

607
Kijiji ni Kawamara
Kukiona ni ishara
Kigarama ipo bara
Wameshaikaribia.

608
Kusikia wakatoka
Kawamara wakafika
Hapo wakatelemka
Ufukweni wakatua.

609
Wakajenga nyumba zao
Kwa mdndo wa kikwao
Kwa matete na mapao
Mshonge wakazinua.

610
Wenyeji wakawajia
Wapate kuwangalia
Pia kuwasaidia
Malazi kujijengea.

611
Kila mume akajenga
Nyumba atakamopanga
Na kafara kwa wahenga
Kila siku kutolea.

612
Waume kwisha kujenga
Na kila kitu kupanga
Wakawa watangatanga
Porini kujiwindia.

613
Na wanyama wakiua
Nyakiru humpada
Naye nyama huitoa
Wenyeji kuwagawia.

614
Hivyo akapendwa sana
Na wazee kwa vijana
Wakamba “Hatujaona
Mtu mwema kuzidia”.


Taswira