Cover Image
close this bookDhima ya kamusi katika kusanifisha lugha (Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, 1995, 118 p.)
View the document(introduction...)
View the documentDibaji
View the documentLahaja Na Mitindo Katika Kks
View the documentFasili Za Vidahlzo Vya Kamusi Ya Kiswahili Sanifu
View the documentUsanifu Wa Vidahizo Vya Kamusi Ya Kiswahili Sanifu
View the documentDhima Ya Kamusi Katika Kufundisha Na Kujifunza Kiswahlli 1
View the documentVipengele Vya Kisarufi Katika Kamusi YA Kiswafflli Sanifu
View the documentVipengele Vya Kimsamiati Katika Kamusi Ya Kiswahili Sanifu
View the documentUtoshelevu Wa Fasili Na Visawe Vya Vidahizo Katika Kamusi Ya Kiswahlli Sanifu1
View the documentKinyume

Dhima Ya Kamusi Katika Kufundisha Na Kujifunza Kiswahlli 1

I. Mbaabu

Utangulizi

Tunapoyatoa maoni na mapendekezo yetu kuhusu njia za kuisahihisha Kamusi ya Kiswahili Sanifu KKS, inafaa tuwakumbuke Watanzania wawili waliosahauliwa na historia licha ya kuiwekea KKS msingi imara. Ndugu Samwel Chiponda aliyekuwa mfanyakazi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Ndugu Abdulla Mohamed el Hathramy kutoka Idara ya Elimu Zanzibar wakishirikiana na Makasisi J.S. Lemble wa Tanganyika na G.W. Broomfield2 wa Zanzibar pamoja na maafisa wa utawala Frederick Johnson3 wa Tanganyika na P. Sheldon wa Zanzibar ndio walikuwa wanachama wa Kamati ya Usanifishaji wa Kiswahili iliyokamilisha kikao chake mjini Dar es Salaam tarehe 9 Oktoba, mwaka 1925. Bila shaka maoni ya Ndugu Chiponda na Hathramy pamoja na ujuzi wao wa Kiswahili uliwaongoza wanachama wengine ambao wote walikuwa Wazungu.

Kamati ya Ndugu Chiponda na wenzake ilitoa mapendekezo kumi na tisa (19) kuhusu njia za kusanifisha Kiswahili. Mapendekezo hayo yalipelekwa kwa serikali za Tanganyika, Kenya, Zanzibar Burundi na Zaire (Congo), mabalozi kadhaa, Chuo Kikuu cha London - School of Oriental and African Studies (SOAS) na Chuo Kikuu cha Witwatersrand cha Afrika ya Kusini, mashirika ya kutafsiri Biblia pamoja na mabingwa wa Kiswahili na lugha za Kibantu wa wakati huo kama vile Sir H.H. Johnson na Profesa Carl Meinhof. Katika pendekezo nambari 12 kamati ilionelea ni bora kurahisisha tahajia za Kiswahili na kuwa na utaratibu maalum wa kuyaandikia maneno ya Kiswahili ili kuepukana na hali ya kuwepo na njia mbili au zaidi za kuliandika neno moja. Zifuatazo ni baadhi ya tahajia zilizopendekezwa na kamati hiyo.

dhoruba

badala ya

dharuba

heshima

badala ya

hishima

hekima

badala ya

hikima

methali

badala ya

mithali

ishirini

badala ya

asharini

lakini

badala ya

ilakini

merikebu

badala ya

marikebu

hesabu

badala ya

hisabu

tisini

badala ya

tisaini

hasa

badala ya

haswa

sheria

badala ya

sharia

asili

badala ya

asli

labda

badala ya

labuda

sharti

badala ya

sharuti

nchi

badala ya

inchi

Kama tutakavyoeleza baadaye, baadhi ya mapendekezo haya hayakuzingatiwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) katika kuitunga KKS licha ya TUKI kuwa mrithi wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambayo iliundwa kufanikisha mapendekezo ya Kamati ya Ndugu Chiponda na wenzake. Baada ya mkutano huo wa usanifishaji wa Kiswahili kulikuwa na mashauriano na mikutano kadhaa kati ya serikali za Afrika Mashariki kabla ya kuanzishwa kwa kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki katika mwaka 1930, Mmoja kati ya mikutano hiyo ni mkutano wa 1928 mjini Mombasa ambao ulikubaliana na mapendekezo ya kamati ya Ndugu Chiponda na wenzake Mapendekezo hayo yalikuwa ni pamoja na pendekezo la kwanza la kutumiwa kwa lahaja ya Kiunguja "pamoja na marekebisho yatakayohitajika" kuwa msingi wa Kiswahili sanifu.

Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na Makao Makuu yake Dar es Salaam kati ya 1930 na 1942 ilipohamia Nairobi. Mwaka 1952 ilihamia Kampala hadi 1962 ilipohama tena hadi Mombasa. Mwaka uliofuata kamati ilihamia Dar es Salaam tena. Mwaka 1964 kamati ilivunjwa na badala yake kikaanzishwa Chuo cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili ambacho kiligeuza jina kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Taasisi haikurithi vitaa na baadhi ya shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki tu, hali ilirithi wafanyakazi wa Kamati wakiwemo Wilfed Whiteley, aliyekuwa Mkurugenzi wa kwanza wa TUKI. Katibu wa mwisho wa Kamati, Jan Knappert. pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa mwisho wa kamati J.W.T. Allen pia ni baadhi ya wafanyakazi wa Kamati walioajiriwa na Taasisi5

Dhima ya kamusi sanifu ni kusanifisha lugha

Kwa watu wengi, wakiwemo walimu na wanafunzi wa lugha, muamuzi wa mwisho wa kutegemewa kuhusu masuala ya tahajia, maana na sarufi (kama vile ngeli za nomino) ni kamusi sanifu ya lugha hiyo. Ubora wa kamusi mara nyingi hutegemea jinsi inavyoweza kuyashughulikia vilivyo masuala hayo. Kwa sasa KKS inao upungufu wa maneno yanayotumiwa sana. Mtu yeyote anayejifunza lugha huvunjika moyo anapoyakosa maneno anayotarajia kuyapata katika kamusi. Ili kuwaridhisha watumiaji wengi, kamusi sanifu haina budi kuwa na maneno mengi katika nyanja nyingi iwezekanavyo. Baadhi ya istilahi za sayansi na teknolojia zinazotumika na watu wengi zinastahili kuwa katika kamusi kuambatana na maendeleo ya jamii. Maana za istilahi hizo zinastahili kuelezwa bila ya kuegemea mfumo wowote wa siasa.

Tatizo kubwa zaidi analokumbana nalo mwalimu na mwanafunzi wa Kiswahili anapoitumia K.K.S ni ule ukosefu wa uamuazi kuhusu usanifu wa tahajia. KKS inayo maneno mengi ambayo yamepewa tahajia zaidi ya moja. Ziko jozi za maneno kama vile sharia - "tazama sheria"; desturi "pengine dasturi"; hesabu - "pia hisabu". Kwa kutumia maneno yenye kuonyesha shaka kama vile "tazama", "pia", na "pengine" KKS inampotosha mwanafunzi. Mwanafunzi wa Kiswahili anayo haki kutarajia KKS impatie tahajia sanifu za maneno ya kawaida badala ya jozi kama glopu/globu, drili/dereli, na spitali/hospitali. Vile vilejozi hizi za tahajia ndizo zilikataliwa na kamati ya ndugu Chiponda na wenzake zaidi ya miaka hamsini kabla ya kutungwa kwa KKS.

Bila shaka tofauti za kirnatamshi kutegemea mazingira ya mtu binafsi na lahaja yake zipo na zitaendelea kuwepo kwa lugha yoyote ile. Hata hivyo kamusi rasmi ya lugha sanifu inalo jukumu la kusanifisha maandishi kwa kutumia tahajia sanifu. Katika utangulizi wa KKS imeelezwa kwamba "maneno katika kamusi hii yameandikwa kufuatana na tahajia sanifu"6 . Hivyo ndivyo kamusi rasmi ya lugha sanifu inavyopaswa kuwa. Utangulizi huo unaendelea:

Maneno pia, pengine na taz yametumiwa kuonyesha hali hiyo7 Kwa yale maneno yenye tahajia zaidi ya moja basi tahajia zote zimeonyeshwa.

Hebu sasa tuyachunguze maneno hayo yanayotumiwa kuonyesha tahajia mbili zilizoko katika KKS. Maneno pia, pengine na tazama yanaonyesha haJi ya kukosa uamuzi. Kusanifisha lugha ni kutoa uamuzi inavyohitajika. Kwa kuyatumia maneno hayo KKS inaonyesha kwamba haina uhakika ikiwa neno sanifu ni desturi na dasturi; hesabu au hisabu. Neno tazama lamwelekeza anayetumia kamusi kwa neno ambalo KKS inalitambua zaidi. Ukiangalia neno markebu unaongozwa: "tazama merikebu"; sharia "tazama sheria"; dharuba tazama dhoruba". n.k. Hivi ni kuonyesha kwamba (labda) KKS inatambua tahajia merikebu, sheria hekima na dhoruba, kuwa sanifu zaidi kuliko markebu, sharia, hikima na dharuba. Ikiwa ni hivyo basi, yaonyesha kwamba neno la mwisho dharuba lililo- kataliwa mwaka 1925 ndilo KKS imeamua kwamba ni zuri zaidi kuliko dhoruba lililosanitishwa. Mwanafunzi wa Kiswahili hana budi kuyapima maneno yote mawili na kuamua ni tahajia ipi atakayoitumia. Mara nyingi tahajia atakayoamua kutumia ni ile anayoshauriwa na KKS kwa neno "tazama". Kwa mujibu wa kamusi hii. nwanafunzi anaweza kuchagua tahajia yoyote na kuitumia kwa kuwa KKS haijamsaidia kutoa uamuzi huo. Wanafunzi tofauti waweza kuchagua tahajia tofauti na tahajia aliyoichagua mwalimu wao. Je huku si ni kuilemaza lugha?

Suala jingine ambalo linazushwa na dondoo la hapo juu kutoka KKS, pamoja na matumizi ya maneno hayo yenye kuzusha shaka kwa mwalimu na mwanafunzi wa Kiswahili ni iwapo tahajia zote mbili zimesanifishwa kama inavyodaiwa katika utangulizi huo wa KKS. Kamati ya usanifishaji wa Kiswahili ya Ndugu Chiponda na wenzake iliamua tahajia za baadhi ya maneno ziandikwe kama tulivyotaja katika utangulizi, kwa mfano desturi, hekima, merikebu na dhoruba. Je ni kikao kipi cha Kamati ya Kiswahili ya ya Afrika Mashariki kilichoamua kwamba tahajia dasturi, hikifna na marikebu ni sanifu baada ya kukataliwa 1925? Vilevile tunashuku iwapo ni kweli kwamba tahajia dasturi, hikima, marikebu, dharuba, chandalua, dereli, glopu, spitali, halambee, chokra, dreva, mazowea, finika na mengine mengi kama hayo yalisanifishwa.

Nyingi kati ya tahajia zilizoorodheshwa juu hazipatikani katika kamusi sanifu ya Kiswahili-Kiingereza iliyotungwa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki chini ya uongozi wa katibu wake Frederick Johnson. Yaelekea kwamba tahajia hizi ni maoni ya watunzi wa KKS wala si maoni ya Kamati iliyokisanifisha Kiswahili. Kama tujuavyo TUKI haijawahi kuwa na vikao vya kimataifa vya kusanifisha maneno ya kawaida ya Kiswahili kama walivyosanifisha istilahi za taaluma mbalimbali. Iwapo hatuna sababu maalum na ushahidi wa kutosha kwamba tahajia hizo zote zilisanifishwa, yafaa ziondolewe kabisa katika KKS. Wakati umewadia wa kuifanya KKS kuwa kielelezo cha Kiswahili sanifu. Wanaosanifisha lugha wanalo jukumu la kutofautisha kati ya tahajia sanifu na zisizo sanifu. Ni maoni ya mwandishi kwamba jukumu hili sasa liko mikononi mwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili kama warithi wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Baadhi ya maneno yenye zaidi ya tahajia moja yamekopwa kutoka lugha ya kigeni, hasa Kiingereza. Taasisi inayafahamu maneno hayo ya Kiingereza. Inajua nl tahajia ipi inayoshabihiana zaidi na neno asilia (neno lililokopwa). Kwa mfano maneno spitali na hospitali yamekopwa kutoka neno hospital la Kiingereza. Taasisi inakerwa na nini ndipo ikope spitali, na glopu, na kusanifisha badala ya kukata yamuzi mara moja kukopa hospitali na globu pekee? Ni nani katika lahaja sanifu ya Kiswahili anayetumia neno halambee? Ikiwa ni matamshi ya hara, mbona basi matamshi harambee linalotumiwa na baadhi ya Wakenya wa bara lisiongezwe? Kwa utupi, msimamo thabiti kuhusu usanifishaji wa tahajia za Kiswahili unahitajika.

Kila anayejifunza lugha ngeni, mathalani Kiingereza hufanya jitihada za kujifunza tahajia kama vile saw (ona), sew (shona), sow (panda), soul (roho) n.k. Lakini kuhusu lugha yetu ya taifa KKS haijali ikiwa tutaandika drili au dereli. Kuruhusu na kupendekeza Kiswahili kiandikwe kiholela "taz, horera", - kadri mtu anavyotaka ni kushusha hadhi ya Kiswahili na dhana nzima ya usanifishaji. Baadhi ya hizi tahajia za ziada bila shaka ni matamshi ya kilahaja au ya tabaka mbalimbali za waliosoma na waliokosa elimu ya kutosha kuweza kutambua asili halisi ya neno lililokopwa. Kwa hivyo inapendekezwa kwamba tahajia moja sanifu itumiwe kwa neno moja. Ikiwa ni lazima, KKS inaweza kuwafahamisha wasomaji wake kwamba badala ya kutamka neno hospitali, kwa mfano, baadhi ya watu hutamka spitali. Lakini ni sharti ifahamike waziwazi kwamba tahajia sanifu ni moja na tahajia hiyo ndiyo pekee inayostahili kuorodheshwa katika kamusi ya Kiswahili Sanitu.

Umuhimu wa kuidurusu kamusi

Nijambo la kawaida kuidurusu kamusi upya kila baada ya muda maalum. Kwa lugha inayoendelea kukua na kupanua msamiati wake kwa haraka kama vile Kiswahili, muda huo haupaswi kuzidi miaka kumi. Mbali na kuongeza maneno mapya katika hilo toleo jipya, fursa hiyo hutumiwa

(1) Kurekebisha makosa yoyote ambayo huenda yalitokea katika toleo lililotangulia, na
(2) Kuandikiana mkataba mpya kati ya watungaji kamusi na wachapishaji8

Huu ni mwaka wa kumi na tatu tangu KKS ichapishwe kwa mara ya kwanza (1981). Ni jambo lisilozusha ubishi kwamba tayari KKS imepitwa na wakati. Njia mojawapo ya kuthibitisha ukweli huu ni kutazama makala yoyote kutoka Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ukiwemo ucangulizi wa KKS yenyewe. Baadhi ya maneno yaliyotumiwa katika utangulizi huo, kama vile kitomeo, vitomeo na kidahizo hayakuorodheshwa katika KKS. Mifano mingine ni maneno kama vile ikama na kasma9, pamoja na neno leksikografia lililotumiwa katika ukurasa wa kwanza wa barua ya Dkt. Mdee ya kutangaza warsha hii. Pengine maneno hayamo katika kamusi kwa kuwa ni maneno ya kitaaluma au istilahi. Wakati umewadia kuamua ni istilahi zipi zitakazokuwepo kwenye kamusi ya kawaida kama KKS na zile ambazo zitaingizwa katika kamusi maalum za taaluma mbalimbali. Maoni ya mwandishi ni kwamba baadhi ya istilahi za taaluma nyingi zinastahili kuwa katika KKS kwa kuwa idadi ya watu ambao wanahitaji kuzifahamu inaendelea kuongezeka kwa haraka kuambatana na maendeleo ya nchi zetu kielimu na kiteknolojia. Neno laweza kuwa la kitaaluma leo, na kesho likawa la kawaida. Hairidhishi kuyaacha nje maneno kama hayo ati kwa sababu ni ya kitaaluma huku yakiendelca kutumiwa katika mawasiliano ya kawaida.

Maneno mengine ya kawaida kama vile nyanja na nyayo ambayo ni nomino za hali ya wingi wa ngeli ya 14 (u) hupatikana lu katika hali ya umoja - uwanja na wayo. Hata ingawa ni sahihi kuyaorodhesha hivyo, hapana shaka kuwa wapo wanafunzi wengi wanaoitumia kamusii hii ambao hawajui watayapata wapi maneno kama hayo. Haitoshi kutoa maelezo hayo katika utangulizi kwa sababu pengine mtu hadewi asili au hali ya umoja wa neno analolitafuta. Mwanafunzi wa Kiswahili atafaidika sana iwapo maneno kama hayo yataorodheshwa katika KKS na kumfahamisha kwamba neno hilo ni nomino ya hali ya wingi na kwamba maana yake inapatikana katika nomino (nomino yenyewe itajwe) ya hali ya umoja.

Kamusi sanifu ifafanue lugha wala isifungamane na itikadi

Kamusi ya Kiswahili Sanifu ilipokuwa ikiandikwa, siasa za ujamaa zilikuwa zikivuma sana nchini Tanzania. Yaonekana kwamba TUKI ilijitwisha mzigo wa kufafanua na kusambaza siasa hizo kupitia KKS. Kwa mfano, maana moja ya neno kabaila imeelezwa kuwa:

Mnyonyaji mwenye majumba mengi ya kupangisha na ardhi kubwa ya kupangisha au inayolimwa na watu wengine wengi kwa ajili ya faida yake.10

Neno linalomtisha na kumkera yeyote anayoitumia KKS katika kufundisha au kujifunza Kiswahili ni Mnyonyaji. Kwa kutumia neno mnyonyaji TUKI iliwashauri (na ingali yaendelea kuwashauri) Watanzania na wengine wanaoitumia kamusi hii wasiutafute utajiri wa aina hiyo kwa kuwa wakiwa na majumba ya kupangisha watakuwa wanyonyaji (sawa na kupe) wanaowanyonya wateja wao. Neno mnyonyaji halijaorodheshwa, kwa hivyo itabidi utafute kitenzi nyonya ndipo upate maelezo kwamba ni "kuishi kwajasho la mwingine".

Maelezo hayo yanampotosha mwanafunzi. Ili kuwa na majumba mengi ya kupangisha ni lazima mtu awe na mali ili aweze kuyanunua au kuyajenga. Kama tujuavyo, ni nadra sana kupata mali halisi bila jasho. Je, mwenye majumba hayo anaishi kwa jasho la nani? Ni maoni ya mwandishi kwamba kizazi cha sasa kinachotumia KKS kimedhulumiwa na TUKI kwa kutishwa kwamba wakitajirika watakuwa wanyonyaji. Dhutuma hii ingeondolewa endapo maelezo yasiyoegemea siasa za upande wowote yangeanzia: "mtu mwenye majumba mengi..."

Mfano mwingine kama huo ni neno bepari. Maana moja ya neno bepari inaelezwa kuwa "mmojawapo katika tabaka la wanyonyaji"10 Misemo ya siasa hizo imetapakaa kote katika KKS. Mifano mingine ni kama vile "ubepari ni unyama" "Ubwanyenye Uchwara:"11 na "Usiwe kupejitegemee"12. Mifano hii michache inazusha suala la ikiwa siasa na propaganda zinazoweza kubadilika wakati wowote ule zinastahili kuingizwa katika kamusi. Kamusi hii hutumiwa zaidi na wanafunzi kuliko watu wazima. Vile vile kamusi hii yaelekea huuzwa nakala nyingi zaidi nje ya Tanzania kama vilc Kenya kuliko vile inavyouzwa Tanzania. (Kufikia 1989 ilikuwa imechapwa upya matoleo 13 nchini Kenya zikilinganishwa na matoleo mawili tu, (1981 na 1988 nchini Tanzania). Inapendekezwa kwamba KKS isahihishwe kwa kutoa maelezo ya maneno ya Kiswahili bila ya kueneza siasa.

Maneno yaliyotoholewa kutoka lugha nyingine

Ukopaji wa maneno ni mojawapo ya njia za kuongeza manepo ya lugha. Kila lugha hukopa maneno kutoka lugha nyingine. Mengi kati ya maneno ambayo Kiswahili kimekopa yanatokana na lugha ambazo zimeingiliana na Kiswahili kama vile Kiarabu, Kihindi, Kiajemi, Kireno na Kiingereza. Mengi kati ya maneno yaliyokopwa na Kiswahili ni maneno ya vitu, dhana au vyombo vipya ambavyo havikuwepo katika utamaduni wa Waswabili. Ni nadra sana kwa lugba yoyote ile kukopa maneno ya msamiati asilia ambayo hutarajiwa kuwa katika kila lugha kama vile maji, mwezi, nyota, mkono, kichwa na jua.

Kamusi ya Kiswahili sanifu imekopa maneno ya Kiingereza kupindukia. Tazama mifano ifuatayo:

sentafowadi

hedimistresi

zigizaga

steshenimasta

chakuleti

speapati

bucha

katekista

kondrati

bradha

Mifano hii (michache) inazusha masuala kadhaa. Je, ikiwa tutakopa steshenimasta mbona tusikope piimasta (P.E. Master), domitorimasta (dormitory master), sabjektimasta (subject master) n.k. Iwapo tutakopa neno bucha (duka la nyama), mbona tusikope fama (mkulima). travela (msafiri), sing'a (muimbaji) na maneno mengine kama vile weka (mfanyakazi)? Jambo linalosisitizwa hapa ni kwamba kukopa kuna mipaka yake. Tukikopa bila mpango itatubidi kulipa kwa kuipoteza lugha tuliyotarajia kuitajirisha kwa lcukopa. Mwanafunzi wa Kiswahili ataridhishwa na ukopaji wa istilahi kama vile aspirini, bakteria na katheta, lakini atashangazwa na sababu za kukopa baadhi ya maneno ya kawaida. Azimio nambari mbili (2) la Kamati ya Usanifishaji wa Kiswahili ya Ndugu Chiponda na wenzake, (1925) lilipendekeza kutumiwa kwa maneno yenye asiJi ya Kibantu kila inapowezekana katika shughuli za uundaji wa maneno mapya ya Kiswahili. Je. tumeridhika kwamba hatuwezi kupata maneno yenye asili ya Kibantu ndipo tukope maneno kama zigizaga na bucha?

Mzizi wa Kitenzi cha Kiswahili

Mzizi wa kitenzi cha Kiswahili ni ile sehemu ya kitenzi inayobeba maana ya kitenzi hicho. Mzizi ni sehemu ambayo haibadiliki, na ambayo haipasuliwi na viambishi awali au viambishi tamati katika myambuliko. Mzizi wa kitenzi chenye asili ya Kibantu ni ile sehemu ya kitenzi ambacho hakijanyambulishwa inayotangulia irabu a ya mwisho ya kitenzi hicho. Vitenzi vyote vyenye asili ya Kibantu huishia kwa irabu (kiishio) a kabla havijanyambulishwa. Mbali na maelezo hayo hatuwezi kusahau kwamba Kiswahili kinazo kanuni zake za mfumo wa sauti unaosababisha mabadiliko ya sauti. Mfumo huo ndio unatuwezesha kuelewa kwamba k hubadilika ikawa sh katika mifano kama vile:

amka

amsha

mka

rusha

pika

mpishi12

Kamusi ya Kiswahili sanifu inatoa mifano kama vile kau kuwa ndio mzizi wa kauka; toro kuwa mzizi wa toroka na mifano mingine mingi, hasa ile inayoishia kwa konsonanti k. Labda waandishi wa KKS walipoamua kutumia mizizi hiyo walikiri kubanwa na maelezo ya neno mzizi kwamba haubadiliki. Neno amsha linapoundwa kutokana na neno amka au (ku) rushwa kutokana na ruka hatuwezi kusema kwamba kiini hubadilika kwa kuwa k ndiyo huwa sh na mabadiliko hayo yanatar.ajiwa katika mazingira hayo ya mfumo wa sauti ya Kiswahili. Dhana ya mzizi wa kitenzi kama inavyojidhihirisha katika KKS inahitaji kuchunguzwa upya. KKS ina mifano ya mizizi kama vile kaz (mzizi wa kaza na kazan (mzizi wa kazana)13. Bila shaka kuna tatizo hapa kwa kuwa maneno yote mawili yana mzizi sawa. Tatizo hili iinatokana na matumizi ya 'kiambishi' - hasa "kiambishi tamati" - ambacho ni sehemu ya kitenzi inayopatikana baada ya mzizi kama vile pigia, pigika, pigisha, pigiwa n.k.

Kiambishi tamati kwa hakika ni kiungo cha kauli kama vile kutendea, kutendeka na kutendana. pamoja na kiishio kama vile irahu a. Sehemu hizi mbili, yaani kiungo cha kauli na kiishio zikitambuliwa vilivyo labda tatizo hili la mzizi litatatuliwa. Viungo vya kauli ya kutendeka - k, ik, ek, lik na lek - vyote huwa na konsonanti k kutangulia kiishio u. Hii ndiyo sababu mizizi ya vitenzi vinavyoishia k hufikiriwa kwamba ni vitenzi vya kauli ya kutendeka. Jambo hili likitambuliwa KKS itakuwa na mizizi iliyo sahihi kama vile kauk mzizi wa kauka na torok-mzizi wa toroka kwa kuwa kauka na toroka ni vitenzi mbavyo bado havijanyambulishwa.

Pia yafaa ikumbukwe kwamba vitenzi vilivyokopwa havina mizizi sawa na vitenzi vyenye asili ya Kibantu. Mofolojia ya vitenzi hivyo ni tofauti na ya vitenzi asilia kwa kuwa neno zima ni mzizi. Kwa mfano, neno safiri likinyambulishwa hutoa maneno kama vile:

msafiri

wasafiri

waliosafiri

usafiri

usafirishaji

kusafirisha

Kwa hivyo KKS haina msingi wala sababu za kutosha kuvunja neno safiri na kueleza kwamba safir ndio mzizi wake. Mifano mingine ni kama vile hubiri lililopewa mzizi hubir, tahiri lililopewa mzizi tahur na samehe lililopewa mzizi sameh.

Hitimisho

Katika kumalizia, ni wazi kwamba KKS ina historia ndefu na inastahili kujitajirisha na misingi iliyowekwa ha kamati ya usanifishaji ya Ndugu Chiponda na wenzake pamoja na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kamusi zake. Pia mwandishi anatoa pongezi zake kwa serikali ya Tanzania kwa kuianzisha na kuikimu Taasisi ya Uchunguzi wa Kishwahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na wafanyakazi wa Taasisi kwa kazi yao ya kujitolea kwa dhati kuhudia ulunwengu mzima wa Kiswahili.

Maelezo

1. Huu ni upanuzi wa Makala ya Mwandishi "Uchambuzi wa Kamusi ya Kiswahili sanifu" iliyochapishwa katika UFUMBUZI toleo la tatu 1989: 26-32.

2. Mwandishi wa Sarufi ya Kiswahili. London: Sheldon Press, 1931.

3. Aliyekuwa katika wa Kwanza wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

4. Rejea F, Johnson. "Report of the Committee for the Standardization of Swahili Language" barua aliyowaandikia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Elimu, Dar es Salaam, Oktoba 16, 1925.

5. Tazama Ireri Mbaabu: Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili. Longman Kenya Ltd. 1991.

6. TUKI 1981. Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: OUP.

7. ibid

8. Kwa kila toleo wachapishaji wanastahili kuongeza asilinua ya malipo wanaowalipa waandishi wa Kamusi hadi kufikia asilimia 50 na pengine asilimia 60 ya mauzo yote.

9. Mbaabu 1991: 116

10. TUKI 1981: 94.

11. ibid: 18

12. Tazama Ireri Mbaabu: Sarufi za Kiswahili. Longman Kenya Ltd. 1992: 158-164.

13. TUKI 1981: 105