Cover Image
close this bookFasihi, Uandishi na Uchapishaji (Dar Es Salaam University Press, 1993, 260 p.)
close this folderSEHEMU YA KWANZA: UWAVITA
View the document1. Historia na Maendeleo ya Umoja wa Waandishi Vitabu Tanzania (UWAVITA)
View the document2. Maaumio ya Washiriki wa Semina ya Kitaifa ya Waandishi na Wahakiki wa Vitabu Iliyofanyika Dar es Salaam 26 - 29 Octoba, 1987

2. Maaumio ya Washiriki wa Semina ya Kitaifa ya Waandishi na Wahakiki wa Vitabu Iliyofanyika Dar es Salaam 26 - 29 Octoba, 1987

1. Ili kuhamasisha uandishi na kuipa fani hii uhai unaostahili UWAVITA unaazimia kuendesha mashindano ya mara kwa mara ya uandishi.

2. Kwa kuwa hakuna sera inayohimiza maendeleo ya uandishi wa vitabu nchini, UWAVITA unapendekeza serikali ianzishe sera hiyo ili isaidie katika ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya uandishi kama vile uchapaji, uchapishaji, na upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya uandishi.

3. UWAVITA unapendekeza kwa wizara na asasi zinazohusika, kwa kadri inavyowezekana, kuteua na kupeleka katika shule vitabu vilivyoandikwa na kuchapishwa Tanzania, na inapotokea kuwa havipatikani, waandishi watafutwe, wahimizwe na kusaidiwa ili watunge vifabu hivyo.

4. Kwa kutambua kuwapo kwa vipaji vya uandishi visivyoendelezwa miongoni mwa Watanzania, UWAVITA unapendekeza kwamba mbinu za utunzi wa vitabu zifundishwe shuleni na vyuoni. Kadhalika semina na warsha kwa ajili ya waandishi chipukizi ziwe zinaendeshwa mara kwa mara na wizara na asasi zinazohusika.

5. Kwa kuzingatia kwamba elimu ni msingi wa maendeleo, na kwamba vitabu ni nyenzo muhimu ya elimu, na kwa kuwa bei za vitabu ni ghali mno kiasi kwamba wananchi walio wengi wanashindwa kuvinunua na kuvisoma, UWAVITA unapendekeza kwamba kodi zinazohusu uchapishaji wa vitabu zipunguzwe au ziondolewe kabisa. Aidha ruzuku zitolewe kwa ajili ya vifaa vya uchapishaji na uchapaji.

6. Kwa kuwa wananchi walio wengi hawapati vitabu kwa wingi na kwa urahisi, UWAVITA unapendekeza maduka ya vitabu, wachapishaji na maktaba kutafuta mbinu nzuri zaidi za kutangaza na kusambaza vitabu kote nchini, kama vile kwa kufanya maonyesho ya vitabu. Aidha, serikali iongeze kasma ya huduma ya maktaba ili iweze kukidhi mahitaji ya wasomaji.

7. Licha ya mchango wao mkubwa, nafasi ya wanawake katika jamii na kadri inavyoakisiwa katika fasihi bado haijatambuliwa ipasavyo. Kwa hiyo UWAVITA unapendekeza: (a) ufanywe utafiti kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili; (b) kuwepo na mipango itakayowawezesha wanawake kukuza vipaji vyao vya uandishi: na (c) waandishi na wasanii wahimizwe kuwasawiri wanawake kwa mtazamo wa kimaendeleo.

8. Kwa kuzingatia upungufu mkubwa mno wa vitabu na magazeti kwa ajili ya watoto na vijana, UWAVITA unapendekeza: (a) ziendeshwe varsha zitakazoshughulikia namna ya kuandika vitabu vya aina hii; (b) ihakikishwe kwamba watoto wanapata vitabu vinavyolingana na utamaduni na desturi zetu; na (c) vitabu vya aina hii vipewe nafasi maalumu katika makadirio ya fedha.

9. UWAVITA unapendekeza kwa vyombo mbalimbali vya habari kutoa umuhimu zaidi kwa uandishi kama vile kwa kuchapisha mapitio ya vitabu vipya na kwa mahojiano na waandishi.

10. UWAVITA unaipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Vijana, na Utamaduni kwa kuwatunza wasanii mashuhuri. Tunapendekeza (a) mpango wa kutuza wasanii uwe wa kila mwaka; (b) UWAVITA ushirikishwe kikamilifu katika uteuzi wa waandishi bora; (c) nyanja zinazotuzwa zipanuliwe ili zihusishe pia shughuli za utafiti na uhakiki; na (d) kima cha tuzo kiongezwe ili kiwiane na hadhi ipasayo.

11. UWAVITA unapendekeza kwa Chama cha Mapinduzi na Serikali kuangalia upya sera ya lugha ili kukuza zaidi matumizi ya Kiswahili katika shule na vyuo vya elimu ya juu.